
Dar es Salaam — Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, leo Jumatano Agosti 13, 2025, ameomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusitisha matangazo mubashara ya kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.
Akiwasilisha ombi hilo mbele ya Hakimu Mfawidhi Franco Kiswaga, Katuga alisema hatua hiyo inalenga kulinda usalama wa mashahidi watakaotoa ushahidi katika kesi hiyo.
“Kuna umuhimu mkubwa wa kulinda mashahidi ili wawe huru kutoa ushahidi bila hofu ya kuathiriwa kutokana na kuonekana hadharani kupitia vyombo vya habari,” alisema Katuga.
Kesi hiyo, ambayo imekuwa ikivutia umakini mkubwa wa umma na kufuatiliwa kwa karibu kupitia matangazo ya moja kwa moja na baadhi ya vyombo vya habari, inaendelea kusikilizwa mahakamani hapo huku pande zote zikiwasilisha hoja.
Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi Agosti 18, 2025, ambapo itatoa uamuzi kuhusu ombi la upande wa Jamhuri la kuzuia urushwaji wa ushahidi mubashara. Upande wa Jamhuri unasema hatua hiyo ni muhimu ili kuwalinda mashahidi wasijulikane, lakini upande wa utetezi unapinga ombi hilo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!