UONGOZI wa klabu ya Yanga inayosimamiwa na Rais Hersi Said wameingia sokoni mapema kuelekea msimu wa 2026/27, ikiwa na lengo la kuimarisha kikosi chake ili kuhimili ushindani wa ndani na kimataifa.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wanaweka mikakati madhubuti ya kuongeza ubora katika maeneo muhimu, huku taarifa kutoka ndani ya klabu zikieleza kuwa kiungo mshambuliaji wa Singida Black Stars, Lamin Jarjou, ni miongoni mwa majina yaliyopo kwenye rada za usajili.
Nyota huyo amevutia vigogo wa Yanga kutokana na kiwango chake bora alichoonyesha msimu huu, ambapo amechangia bao moja na asisti tatu, hali inayomfanya kuonekana kuwa chaguo sahihi kuongeza ubunifu katika eneo la kiungo mshambuliaji.
Inaelezwa kuwa mazungumzo ya awali tayari yameanza kati ya pande hizo mbili, huku benchi la ufundi likivutiwa na sifa zake, ikiwemo kasi, uwezo wa kumiliki mpira na kupiga mashuti ya mbali, mambo yanayoweza kuongeza nguvu mpya kwenye kikosi hicho.
Hata hivyo, iwapo dili hilo litakamilika, Jarjou atakutana na ushindani mkali wa namba ndani ya kikosi hicho chenye majina makubwa, akiwemo Maxi Nzengeli na Duke Abuya ambao tayari wamejijengea nafasi muhimu ndani ya timu.
Mbali na hilo, Yanga pia inadaiwa kumfuatilia kwa karibu mshambuliaji wa TRA United, Ramadhan Chobwedo, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha safu ya ushambuliaji kuelekea msimu ujao.
Hatua hizo zinaonyesha dhamira ya Yanga kuendelea kubaki kileleni kwa kuhakikisha inakuwa na kikosi kipana chenye ushindani mkubwa katika kila nafasi hali itakayoongeza presha chanya kwa wachezaji na kuinua kiwango cha timu kwa ujumla.
The post MPANGO MKUBWA YANGA WAANZA KUFICHUKA, USAJILI WENYE KISHINDO WAPANGWA MAPEMA appeared first on Soka La Bongo.











Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!