KIPA wa Yanga, Hussein Masalanga, amesema kuwa uwepo wa makipa wa kigeni katika Ligi Kuu Tanzania Bara haumpei presha yoyote, kwani anaamini kila mmoja yupo uwanjani kutafuta riziki na kuendeleza maisha yake ya soka.
Masalanga ameeleza kuwa kwake hali hiyo ni ya kawaida kabisa, akisisitiza kuwa wachezaji kutoka Tanzania pia huenda kucheza katika nchi nyingine wakitafuta fursa na maisha bora zaidi, hivyo hakuna sababu ya kuona tofauti.
Ameongeza kuwa soka la kisasa limekuwa la kimataifa zaidi, ambapo ligi nyingi duniani hujumuisha wachezaji kutoka mataifa mbalimbali, jambo linalochangia kuongeza ushindani na ubora wa mchezo.
“Binafsi kwangu hawajaniongezea presha wala kunipa changamoto yoyote ya ziada, wamekuja kutafuta maisha kama ilivyo sisi. Kikubwa ninaona uwepo wao ni fursa ya kujifunza mambo mapya,” amesema Masalanga.
Kipa huyo amesema ushindani uliopo ndani ya kikosi chao unawasaidia makipa wote kujituma zaidi mazoezini na uwanjani ili kuhakikisha kila mmoja anakuwa katika kiwango bora muda wote.
Masalanga ameweka wazi kuwa anaheshimu uwezo wa makipa wote waliopo ligi kuu, akiamini kila mmoja ana mchango wake katika kukuza kiwango cha soka nchini.
Akizungumzia ubora wa makipa, Masalanga hakusita kumtaja Djigui Diarra kuwa ni miongoni mwa makipa bora, ameeleza kuwa uzoefu na kiwango chake cha juu kinamfanya kuwa mfano mzuri wa kuigwa ndani na nje ya uwanja.
The post KIPA YANGA AFUNGUKA, WAGENI SIO TISHIO NI FURSA appeared first on Soka La Bongo.











Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!