WINGA wa Simba, Anicet Oura, ameendelea kuwa tishio uwanjani, hali iliyomfanya beki wa Yanga, Israeli Mwenda, kutoa tahadhari kwa mabeki wenzake kuhakikisha wanakuwa makini wanapokutana naye.
Kauli hiyo inaashiria kuwa safu ya ulinzi ya Yanga tayari imeanza kuweka mikakati ya mapema kwa ajili ya kumdhibiti Oura kabla ya mchezo wao dhidi ya Simba utakaochezwa Mei 3, 2026, katika Kariakoo Derby ya mzunguko wa pili.
Katika mchezo wa duru la kwanza, Yanga walipokuwa nyumbani walilazimishwa sare tasa dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, matokeo yaliyoonyesha ushindani mkubwa kati ya timu hizo mbili.
Mwenda amesema kuwa kutokana na ubora wa mawinga wengi katika ligi, wakati mwingine inakuwa vigumu kupima kiwango chao halisi, hasa pale timu yao inapokuwa na umiliki mkubwa wa mpira.
Hata hivyo, ameweka wazi kuwa Oura ni miongoni mwa wachezaji hatari wanaohitaji umakini wa hali ya juu kwa sababu ya mbio zake za kushtukiza ambazo zinaweza kuleta madhara kwa mabeki wasipokuwa makini.
“Katika mechi dhidi ya Simba, yule winga (Oura) ana mikimbio ya hatari sana. Mchezaji usipokuwa makini, anaweza kukuacha kirahisi,” amesema Mwenda.
Ameongeza kuwa ili kumdhibiti mchezaji wa aina hiyo, ni muhimu kuwa na umakini wa muda wote kwa kufuatilia mwenendo wake uwanjani, ikiwemo kusoma harakati zake mapema kabla hajaleta madhara.
Mwenda amesema katika baadhi ya mechi za ligi, ni vigumu kuona ubora wa mchezaji mmoja mmoja kutokana na timu yao mara nyingi kuwa na umiliki mkubwa wa mpira, hali inayoficha uwezo halisi wa wapinzani.
The post OURA AWASHTUA YANGA, SAFU YA ULINZI YAINGIA KAZINI MAPEMA appeared first on Soka La Bongo.











Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!