Na Mwandishi Wetu
Ubalozi wa Italia nchini Tanzania kwa kushirikiana na Wakala wa Biashara wa Italia pamoja na Karimjee Group, umetangaza kuadhimisha Siku ya Ubunifu wa Italia Duniani 2026 (IDD) kupitia maonesho maalum ya sanaa na ubunifu yanayoitwa “Glass Bridge – Murano Meets Shanga” yatakayofanyika jijini Dar es Salaam.
Maonesho hayo yanatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 28 Machi hadi 4 Aprili 2026 katika ukumbi wa Rangi Gallery, yakilenga kuonesha ubunifu unaounganisha utamaduni wa Italia na Tanzania.
Siku ya Ubunifu wa Italia Duniani huandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Italia kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni ya Italia, ikiwa na lengo la kuhamasisha ubunifu na usanifu wa Italia kote duniani. Kaulimbiu ya mwaka huu, ikiwa ni toleo la 10, ni “RE-DESIGN: Regenerating spaces, objects, ideas, relations”.
Maonesho hayo yataangazia mazungumzo ya kipekee kati ya ubora wa ubunifu wa Italia na ustadi wa ufundi wa Tanzania, yakijumuisha taa za kisasa kutoka Foscarini pamoja na vyungu vya kioo vya Murano vilivyotengenezwa kwa mikono, sambamba na kazi za sanaa zinazounganisha mbinu za Murano na Shanga.
Kampuni ya Foscarini, iliyoanzishwa mwaka 1981 katika kisiwa cha Murano, inajulikana kwa kutengeneza taa za hali ya juu zinazochanganya ufundi wa jadi wa kioo na teknolojia ya kisasa. Murano ina historia ndefu ya utengenezaji wa kioo inayodaiwa kuanza karne ya 8 kabla ya Kristo, na hadi leo imeendelea kuwa kitovu cha sanaa ya kioo duniani.
Kwa upande wa Tanzania, maonesho hayo pia yatahusisha kazi kutoka Shanga, taasisi ya kijamii iliyopo Arusha inayowaajiri watu wenye ulemavu kuzalisha bidhaa za mapambo kwa kutumia vifaa vilivyorejelewa.
Kupitia mradi wa “Glass Bridge” ulioanzishwa mwaka 2025 na mbunifu Emmanuel Babled kwa kushirikiana na kampuni yake ya Kukua, mafundi wa Murano wameweza kushirikiana na wasanii wa Shanga kubadilishana ujuzi na kuzalisha kazi za sanaa zinazobadilisha taka kuwa bidhaa zenye thamani ya kisanii.
Mradi huo umeelezwa kuwa daraja la ubunifu linalounganisha tamaduni mbili, huku ukichochea uchumi wa mzunguko na kuhamasisha matumizi endelevu ya rasilimali.
Waandaaji wameeleza kuwa maonesho hayo yatatoa fursa kwa umma kujionea kazi za kipekee zinazochanganya ubunifu wa Italia na Tanzania, pamoja na kununua bidhaa za sanaa zilizounganishwa kwa ubunifu huo.
Umma unahimizwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia ubunifu huo unaobadilisha taka kuwa sanaa na kuonesha nguvu ya ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya ubunifu.











Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!