Search
Sign In
2 Register
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

USUSI WATAJWA KAMA FURSA YA AJIRA KWA VIJANA

  • 14
Scroll Down To Discover

Na Meleka Kulwa- Dodoma

KATIKA juhudi za kupanua wigo wa ajira kwa vijana nchini, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema kazi ya ususi inapaswa kutambuliwa kama ajira rasmi na yenye mchango mkubwa katika kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.

Akizungumza jijini Dodoma katika uzinduzi wa Siku ya Wasusi, Waziri Mavunde alisema ususi ni kazi halali inayoweza kuwatoa vijana, wa kike na wa kiume, kutoka kwenye utegemezi na kuwasaidia kujitegemea kiuchumi.

“Kwa mujibu wa sera ya ajira nchini, kazi yoyote halali inayomuingizia mtu kipato ni ajira. Ususi umeajiri maelfu ya vijana nchini na unapaswa kuungwa mkono, kuboreshwa na kupewa heshima inayostahili,” alisema.

Waziri huyo aliongeza kuwa serikali kupitia Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) imeanza kutoa mafunzo mafupi ya ususi ili kusaidia vijana waliokuwa wakijifunza kienyeji waweze kupata maarifa ya kitaalamu na kujiinua zaidi kiuchumi.

Amesema ipo haja ya kuingiza sanaa ya ususi katika mitaala rasmi ya elimu kuanzia ngazi za chini, ili wanafunzi waweze kuhitimu wakiwa na ujuzi wa kujitegemea, na kusaidia kupunguza tatizo la ajira nchini.

Aidha, alitoa wito kwa jamii kuacha kuwahukumu vijana wa kiume wanaojihusisha na kazi hiyo, akieleza kuwa hakuna kazi ya aibu ilimradi ni halali na inampatia mhusika kipato.

“Nimekutana na vijana wengi wa kiume wanaofanya kazi ya ususi na wanafanya vizuri. Tatizo ni mtazamo hasi wa jamii. Tuwape nafasi na tuwaunge mkono,” alisema.

Katika uzinduzi huo uliofanyika kwa mara ya kwanza jijini Dodoma, wasusi kutoka mikoa mbalimbali walikusanyika kwa lengo la kushirikishana uzoefu, kujenga mtandao wa pamoja, na kuifikia serikali ili waweze kupata mikopo na fursa za uwezeshaji.

Mkurugenzi wa Chido Point, Maria Mwampanga, ambaye ndiye aliyeandaa siku hiyo ya wasusi, alisema bado kuna uhitaji mkubwa wa kuwaunganisha wasusi, kuwapa elimu ya kifedha na kuwasaidia kufikia taasisi za kifedha kwa ajili ya mikopo na mitaji.

Kwa upande wao, baadhi ya wasusi walieleza namna walivyopambana na mitazamo hasi ya jamii kuhusu kazi hiyo, hasa kwa vijana wa kiume, lakini walisisitiza kuwa wamefanikiwa kubadilisha maisha yao kupitia kipaji hicho.

Frenk Mwingira, msusi kutoka Dodoma, alisema alianza kazi hiyo akiwa mdogo baada ya kuiona ikifanywa na mama na dada zake. Alikumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa watu waliodhani kuwa kazi hiyo haifai kwa wanaume, lakini aliamua kufuata kipaji chake.

“Siku hizi watu wameanza kunielewa. Kazi hii imenifanya kuwa msaada mkubwa kwa familia yangu. Wale waliokuwa wananibeza sasa ndio wateja wangu,” alisema.

Naye Faustin Kwolesya kutoka mkoa wa Kilimanjaro alisema alianza ususi mwaka 1997, na wakati huo alikuwa akitengwa hata na viongozi wa dini kwa madai kuwa anakaa na wanawake. Hata hivyo, aliamua kupuuza maneno ya watu na kuendelea na kazi hiyo hadi leo, ambayo imemuwezesha kujikimu na kusaidia familia.

Uzinduzi wa siku ya wasusi umeelezwa kuwa mwanzo wa harakati za kuitambua rasmi sekta hiyo kama chanzo cha ajira endelevu kwa vijana, huku serikali ikihimizwa kuongeza juhudi za kuwezesha mafunzo ya stadi za maisha kwa wananchi wake.



Prev Post Alipambana sana kupata mapenzi ya huyu binti bila mafanikio ila leo hii wapo pamoja
Next Post Israel yashambulia uongozi wa Hamas Doha, Qatar. Katika Dira ya Dunia TV
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook