
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuwa serikali yake itahakikisha madai yote halali ya waliokuwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Karatasi Mgololo (Mgololo Paper Mill) yanalipwa baada ya uhakiki.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Septemba 6, 2025, katika eneo la Nyororo, wilayani Mufindi mkoani Iringa, Samia alisema suala hilo limeshughulikiwa na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, ambaye tayari amesikiliza malalamiko ya wafanyakazi na sasa serikali ipo katika hatua ya kuyahakiki.
“Suala la madai ya waliokuwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Mgololo. Madai haya huko nyuma tulilipa, mwekezaji alilipa, serikali ililipa, lakini bado kumetokea madai mengine. Tumepokea madai, tunakwenda kuyahakiki, na yale ambayo yataonekana ni madai ya halali, serikali italipa. Ndugu zangu hakuna ambaye haki yake hataipata,” alisema Samia.
Aidha, Samia alizungumzia changamoto zinazolikabili Kiwanda cha Chai cha Mufindi (Mufindi Tea and Coffee Company), kinachoendeshwa na kampuni ya DL kutoka Kenya. Alisema kampuni hiyo imekumbwa na changamoto za kibiashara lakini imeanza kulipa sehemu ya madeni yake kwa wakulima na wafanyakazi.
Ameongeza kuwa endapo wawekezaji hao watashindwa kuendeleza mashamba ya chai, serikali italazimika kuyachukua na kuyakabidhi kwa vyama vya ushirika ili kuendeleza uzalishaji.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!