Search
Sign In
2Your Cart
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Rwanda na DRC Watia Saini Mkataba wa Amani Washington

  • 13
Scroll Down To Discover

Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimetia saini makubaliano ya kihistoria ya amani jijini Washington, Marekani, katika hatua inayosifiwa na baadhi kuwa ni mafanikio ya kidiplomasia, lakini inayotazamwa na wakosoaji kama ushindi wa kisiasa kwa waasi wa M23 na zawadi kwa “wavamizi.”

Makubaliano hayo, yaliyosimamiwa na Marekani, Qatar na Umoja wa Afrika, yanaelezwa kuwa jaribio la kurejesha amani katika Ukanda wa Maziwa Makuu, hususan Mashariki mwa DRC, ambako mapigano ya muda mrefu yamesababisha maelfu ya vifo na mamilioni ya watu kuwa wakimbizi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, ambaye alishuhudia hafla hiyo, ameeleza matumaini mapya yanayoletwa na mkataba huo: “Sasa watu wanaweza kuanza kuota ndoto mpya za maisha bora. Tunatambua changamoto zilizopo, lakini huu ni mwanzo wa mwelekeo mpya.”

Mkataba huo unasisitiza kusitishwa kwa kile kilichoelezwa kuwa “hatua za kijihami” za Rwanda, bila kuitaja moja kwa moja M23 — kundi la waasi wa Kitutsi linalohusishwa na Kigali, ambalo limeteka maeneo muhimu ya mashariki mwa DRC, likiwemo jiji la Goma.

Rwanda, kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje, Olivier Nduhungirehe, ilieleza kuwa hatua ya kwanza itakuwa kushughulikia kundi la waasi la FDLR — lililoundwa na baadhi ya Wahutu waliotuhumiwa kushiriki mauaji ya kimbari ya 1994.

“Tunataka FDLR waondolewe kabisa. Tukifanya hivyo, hakutakuwa na sababu yoyote ya hatua za kujihami tena,” alisema Nduhungirehe.

Kwa upande wa DRC, Waziri wa Mambo ya Nje, Therese Kayikwamba Wagner, alisisitiza kuwa makubaliano hayo ni uthibitisho wa dhamira ya kulinda mamlaka ya kitaifa: “Amani ni chaguo, lakini pia ni wajibu wa kulinda uhuru wa mataifa. Tunataka suluhisho la haki, si tu la kisiasa.”

Hata hivyo, si wote waliopokea makubaliano haya kwa mikono miwili. Wakosoaji wa ndani na nje ya DRC wameeleza hofu kuwa mkataba huo unaifanya Kigali kuonekana mshirika halali wa usalama, badala ya mshawishi wa mzozo. Pia kuna maswali kuhusu iwapo makubaliano haya yatazuia urejeo wa M23 au ni mwanzo wa kuhalalisha ushawishi wao.

STORI NA ELVAN SITAMBULI | GPL



Prev Post Mgao wa Bilioni 1.5 Unakusubiri na Lucky Rush Leo
Next Post Rais Dkt Samia Awaapisha Viongozi Wateule Ikulu Chamwino Dodoma (Picha +Video)
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook