

Na Sabina Wandiba
Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), inatarajia kuanzisha huduma ya kuzilipia huduma ya afya kwa familia zisizokuwa na uwezo ili kuhakikisha hakuna Mtanzania anayepoteza maisha kwa kukosa matibabu.
Akiongea katika Mkutano Mkuu wa Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DAR-PC), Meneja Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF) Mkoa wa Temeke, Kigamboni na Zanzibar, Simon Ruvinga alisema kuwa, katika kuhakikisha Watanzania wote wanapata matibabu katika Vituo vya Afya, Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF), tayari imeshaanza mchakato wa kuzipitia kaya za watu wasiokuwa na uwezo na kuziorodhesha ili waweze kuingizwa kwenye utaratibu wakupatiwa matibabu kwa gharama za Serikali.
“Tayari zoezi hilo limeshaanza kufanyika katika baadhi ya maeneo, lengo ni kuhakikisha hakuna Mtanzania atakayepoteza maisha kwa sababu ya kukosa pesa za matibabu,” alisema Meneja huyo.
Aidha ameongeza kuwa, mbali na huduma hiyo kwa wasiojiweza, lakini pia imeanza mchakato wa kuanzisha vifurushi vya Bima ya Afya kwa familia isiyozidi watu nane, ambayo haitagharimu zaidi ya Shilingi. 150,000 kwa mwaka mzima, gharama ambayo inatarajiwa kuwa nafuu sana.
Mbali na kifurushi hicho pia NHIF imeanzisha kifurushi kwa vijana kuanzia miaka 18-35 kwa gharama ya Sh.168,000, pamoja na kifurushi cha watoto cha Sh.50,400, miaka 36-59 kwa Sh. 192,000, wazee Sh. 240,000 pamaoja na kilekifurushi cha watoto kupitia mashuleni, ambacho tayari baadhi ya watoto wameshaanza kunufaika nacho na wanapatiwa matibabu kwa gharama nafuu kwa mwaka mzima.
Amesema, pamoja na muitikio mzuri wa Watanzania kujiunga na Mfuko huo, lakini bado wanaendelea kutoa elimu kwa Wananchi ili waweze kuona umuhimu wa huduma ya Bima ya Afya.
Mfuko unaendelea na maboresho kadhaa ambapo tayari kuanzia mwaka 2024 iliacha kuchapisha Kadi za mashine za Bima ya Afya na badala yake unatumika utaratibu wa mgonjwa kutumia namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA).
Mwisho
Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV — usisahau ku-like, ku-comment na ku-subscribe ili uendelee kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!