Search
Sign In
2Your Cart
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Gachagua Aonya Vijana Kuhusu Maandamano ya Kumbukumbu Juni 25

  • 30
Scroll Down To Discover

Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua.

Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, ametoa tahadhari kali kwa vijana wa taifa hilo kutojitokeza katika maandamano ya kumbukumbu ya mwaka mmoja wa waandamanaji waliouawa wakati wa maandamano ya kupinga ushuru mnamo Juni 25, mwaka jana.

Amedai kuna njama hatari ya kuwaua vijana hao inayoratibiwa na viongozi Fulani wa serikali. Akizungumza kupitia kituo cha redio cha Kameme FM, Gachagua amesema kuwa kwa nyakati tofauti viongozi hao wamekuwa wakiajiri wahuni kwa ajili ya shughuli zao jijini Nairobi, na kwamba kundi hilo ndilo litatumika kuwashambulia vijana endapo watajitokeza kwa ajili ya maandamano ya kumbukumbu hiyo.

“Nina hofu kubwa kwamba vijana wakitoka mitaani, serikali na gavana wa Nairobi watatumia wahuni kutoka maeneo kama Umoja, Kayole na kwingineko kuwaua vijana wetu. Ninaomba vijana wabaki nyumbani. Watawindwa na kuuawa. Sitaki kuona watoto wetu wakipelekwa machinjioni huku sisi wazazi tukitazama.” Ameeleza.

Gachagua pia amewataka wazazi kuwasihi watoto wao kutoshiriki maandamano hayo mitaani, akisisitiza kuwa watu hao wana kiu ya damu ya vijana.

Alienda mbali zaidi akitolea mfano wa vurugu zilizotokea tarehe 12 Juni ambapo maandamano yaliitishwa katikati ya jiji la Nairobi wakitaka kukamatwa kwa Naibu Mkuu wa Polisi, Eliud Lagat, kutokana na kifo cha Albert Ojwang’ akiwa mikononi mwa polisi. Gachagua amedai magari yaliyoteketezwa yalikuwa sehemu ya njama ya serikali kuhalalisha matumizi ya nguvu kubwa ya polisi dhidi ya vijana.

“Hakuna mtu aliyeripoti kuwa gari lake limechomwa. Magari yalifuatiliwa kupitia NTSA na hayakuwa yamesajiliwa kwa mtu yeyote. Ilikuwa njama tu ya kuchochea polisi wawashambulie vijana,” ameeleza.

Kwa upande mwingine, kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, ametoa wito wa wananchi kufika katika majengo ya Bunge mnamo Juni 25 na kuwasha mishumaa kwa ajili ya kuwakumbuka vijana waliouawa au kujeruhiwa mwaka jana.

“Tarehe 25 Juni, Wakenya waende pale lango la Bunge na kuwasha mishumaa kwa heshima ya vijana waliouawa au kujeruhiwa na polisi,” alisema Kalonzo akiwa kwenye ibada huko Kilifi.

STORI NA ELVAN STAMBULI, GPL



Prev Post Waziri Mkuu Mgeni Rasmi Kilele Maadhimisho Ya Miaka 50 Ya TET
Next Post CCM: Atakaepandikiza Ukabila, Udini na Ubaguzi asiachwe atambe
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook