

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni ya utoaji wa msaada wa kisheria bila malipo kwa wakazi wa Dar es Salaam, ijulikanayo kama “Mama Samia Legal Aid”.
Kampeni hiyo itazinduliwa rasmi Juni 16, 2025 katika viwanja vya Maturubai, Mbagala, na itaendelea kwa muda wa siku 10 mfululizo, ikihusisha Halmashauri zote za Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya kisheria bila kikwazo chochote cha kiuchumi. “Napenda niwafahamishe wakazi wa Dar es Salaam kuwa huduma hii muhimu inawalenga moja kwa moja wananchi wa kipato cha chini ambao mara nyingi wamekuwa wakikosa haki kwa sababu ya ukosefu wa msaada wa kisheria,” amesema Chalamila.
Ametaja huduma zitakazotolewa ni pamoja na usaidizi kuhusu masuala ya mirathi, migogoro ya ardhi, ndoa, uandishi wa wosia pamoja na ushauri wa kisheria kwa ujumla. Wanasheria waliobobea kutoka taasisi mbalimbali za kiserikali na binafsi wanatarajiwa kushiriki katika kampeni hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi, ameeleza kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kutoa haki kwa wote unaotekelezwa chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amebainisha kuwa changamoto za kiuchumi na ukosefu wa uelewa kuhusu haki za kisheria kwa wananchi wengi ndizo zilizopelekea Serikali kubuni mkakati huu wa kusaidia wananchi.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!