

Na Mwandishi wetu, Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi kimesema raia kutopiga kura kwa hiari yake si kosa la jinai bali akitokea mtu ,chama au kikundi kinachowazuia watu wasipige kura hilo liitakuwa ni kosa la jinai.
CCM kimesisitiza kuwa hiari ya mtu kutopiga kura ni uamuzi wake ambao haukiuki wala kuvunja katiba na sheria.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis ameeleza hayo na kusema kila mwananchi aliyetumiza masharti ya sheria ana haki ya kupiga kura.
Mbeto alisema kwa mujibu wa Katiba ya Mwaka 1977 Ibara ya 74 chini ya sheria ya Uchaguzi Namba 2 iliofanyikwa marekebisho mwaka 2024 ni kosa kumzuia mtu asipige kura .
Alisema haki ya kupiga kura ni ya kila mtanzania aliyetajwa kwa haki za kiraia hivyo ana wajibu wa kujiandikisha na kuwa mpiga kura.
“Kupiga kura ni haki ya kila raia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kutopiga kura ni hiari ya mtu lakini mtu au watu wakimzuia raia asipige kura hilo litakuwa ni kosa la jinai”Alisema Mbeto
Aidha, Katibu huyo Mwenezi alisisitiza kuwa kuunda genge ,kundi au mtu kuamua kuzuia watu wanaotaka kupiga kura hilo ni kosa la jinai, ingawaje mtu ikiwa hataki kupiga kura hatakabiliwa na jinai .
Hata hivyo Mbeto aliwahimiza wananchi waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Mpige kura kujiandaa na Uchaguzi wa oktoba mwaka huu.
“Hayupo na wala hatokeo mtu mwenye jeuri au ubavu wa kuzuia uchaguzi usifanyike. Uchaguzi wa nchi umetajwa na sheria na katiba ya nchi “Alisema Katibu huyo
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!