
Wakazi wa eneo la Mokwa wameeleza kwa BBC jinsi mafuriko yalivyokumba mji wao kwa ghafla na kusababisha uharibifu mkubwa.
Idadi rasmi ya vifo kutokana na mafuriko mabaya yaliyotokea Alhamisi katika mji wa Mokwa, uliopo katika Jimbo la Kati la Niger, imefikia watu 200, kwa mujibu wa maafisa.
Hata hivyo, watu wengine 500 bado hawajulikani walipo, lakini afisa wa eneo hilo, Musa Kimboku, ameieleza BBC kuwa juhudi za uokoaji zimesitishwa kwa kuwa mamlaka haziamini tena kuwa kuna mtu yeyote aliyebaki hai.
Mafuriko hayo, yanayodaiwa kuwa mabaya zaidi kuwahi kutokea katika eneo hilo kwa kipindi cha miaka 60, yalikumba mitaa ya Tiffin Maza na Anguwan Hausawa baada ya mvua kubwa kunyesha.
Ili kuzuia mlipuko wa magonjwa, mamlaka zimetangaza kuwa zitaanza kufukua miili iliyozikwa chini ya ardhi, kwa mujibu wa mkuu wa wilaya ya Mokwa, Muhammadu Aliyu.
Wakisimulia hali ya maafa, wakazi wa eneo hilo wameeleza BBC kuwa walishuhudia nyumba zao na jamaa zao wakisombwa na maji.Mmoja wao, Adamu Yusuf, alipoteza mkewe na mtoto wao mchanga.
“Niliangalia kwa huzuni maji yakisomba familia yangu. Niliokoka kwa sababu najua kuogelea,” aliieleza BBC.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!