
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Jerry William Silaa (Mb) amesema kuwa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo tayari kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika kuhakikisha malengo ya Mkutano wa Dunia wa Jumuiya ya Habari (WSIS), Jukwaa la Usimamizi wa Intaneti, Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030 na makubaliano yote yaliyoafikiwa kidunia kuhusu masuala ya kidigitali yanafikiwa.
Utekelezaji wa malengo ya kidijitali inatajwa kuwa ni fursa muhimu katika kuchagiza maendeleo ya kijamii,teknolojia,kiuchumi, kielimu na mengineyo.
Ameyasema hayo leo Mei 30,2025 wakati akifungua Mkutano wa 14 wa Jukwaa la Usimamizi wa Intaneti barani Afrika (AfIGF) 2025 kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Dotto Biteko unaoendelea katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Amesema, uamuzi wa Serikali ya Tanzania kuridhia na kuratibu mkutano huo ni ishara tosha kuwa,Serikali imedhamiria kuchochea kasi ya maendeleo katika jamii kupitia intaneti.
“Si tu kwa wananchi wetu, bali pia kwa jamii ya Afrika na duniani kwa ujumla.”
Katika hatua nyingine, Waziri Slaa amesema, Tanzania imeendelea kupiga hatua katika kuhamasisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuchagiza ukuaji wa uchumi wa kidigitali.
Ni kwa kuhakikisha kila sekta inaendesha shughuli zake kidigitali kama njia ya kuongeza ufanisi huku akisisitiza kuwa, jitihada hizo zimewezesha mifumo kusomana na kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali nchini.
Pia, kwa niaba ya Serikali, Waziri Silaa amewaeleza washiriki wa mkutano huo kuwa, uwepo wao hapa Tanzania unawapa fursa ya kujifunza mambo mengi muhimu ambayo si rahisi kuyapata maeneo mengine duniani.
Amesema, jamii ya Watanzania ambayo kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 inakadiriwa kuwa watu zaidi ya milioni 60 imekirimiwa kuwa na utamaduni wa kukirimu vema wageni, upendo na amani.
Pia, amesema ishara hiyo ya upendo na amani kutoka kwa Watanzania inatoa nafasi pana kwa wageni kuweza kwenda popote ikiwemo kujifunza na kufurahia vivutio vya utalii kote Bara na Visiwani.
Vilevile, Mheshimiwa Silaa amewaeleza washiriki hao kuwa, uwepo wao hapa Tanzania ni mwendelezo wa wageni na mataifa mbalimbali kuja Tanzania kujifunza kuhusu masuala mengi ambayo yana mchango mkubwa kwa ustawi wao na jamii zao.
Mkutano huo ambao ni jukwaa la wazi linaongozwa na kauli mbiu ya Kuwezesha Mustakabali wa Kidijitali wa Afrika ambapo umeanza Mei 29,2025 na unatarajiwa kufikia tamati Mei 31, 2025.
Jukwaa hilo limezileta pamoja Serikali na wabunge kutoka mataifa mbalimbali, mashirika mbalimbali na wadau kutoka sekta binafsi ndani na nje ya Bara la Afrika.
Vilevile jukwaa hilo limewaleta pamoja wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), wanazuoni, vijana, vyombo vya habari na wanafunzi.
Lengo la jukwaa hili la kwanza kufanyika hapa nchini ni kujenga ushirikiano wa pamoja katika kuunda sera na mifumo ya kidijitali inayohudumia maslahi ya wote barani Afrika kwa ustawi bora wa huduma za intaneti.
Katika jukwaa hili wataalamu wa masuala ya mtandao barani Afrika wanajadili kwa kina mada mbalimbali ikiwemo Akili Unde (AI) na teknolojia zinazoibuka,miundombinu ya umma ya kidijitali na usimamizi wa takwimu.
Mada nyingine ni kuhusu usalama wa mtandao,ustahimilivu na uaminifu wa kidijitali, upatikanaji na uunganishaji wa huduma za kidijitali na kuimarisha ushirikiano katika masuala ya kidigitali.
Wakati huo huo, Waziri Silaa amewaeleza washiriki hao kuwa, Tanzania imeendelea kuwa kinara katika kutekeleza mageuzi mbalimbali ya kidigitali huku ikiwezesha TEHAMA kufundishwa katika shule kuanzia ngazi za chini hadi juu.
Aidha, Serikali inaendelea kuwaunga mkono Watanzania wenye bunifu hususani vijana ili ziweze kuleta matokeo makubwa kuanzia ajira na kukuza uchumi wao ikiwemo Taifa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo amewahimiza washiriki wa jukwaa hilo kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika kuona umuhimu wa kujifunza lugha ya Kiswahili.
Amesema kuwa, Kiswahili kinatoa uwanda mpana kwa kila anayekifahamu kutambua fursa mbalimbali zilizopo hapa Tanzania huku akiwashauri pia kuona umuhimu wa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii ndani na nje ya Jiji la Dar es Salaam.
Kwa upande wao washiriki na viongozi mbalimbali kutoka nje ya nchi hawakusita kumpongeza Rais Dkt.Samia kwa jitihada zake ambazo zimewezesha Tanzania kupiga hatua kubwa katika TEHAMA.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!