Search
Sign In
2Your Cart
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Wiki ya Asasi za Kiraia (Azaki) 2025 Kufanyika Juni Mount Meru Jijini Arusha

  • 15
Scroll Down To Discover

The Foundation for Civil Society (FCS) imetangaza kuwa Wiki ya Asasi za Kiraia (Azaki) kwa mwaka 2025 itafanyika kuanzia Juni 2 hadi 6 katika ukumbi wa Mount Meru, mkoani Arusha.

Maadhimisho haya yanatarajiwa kukutanisha wadau mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kutathmini mafanikio ya Azaki na kupanga mikakati ya kuimarisha maendeleo ya taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari,kuelekea maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Nesia Mahenge, amesema tukio hilo litakuwa jukwaa muhimu kwa wadau kujadiliana na kushirikiana katika kuleta maendeleo.

“Tunashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wa serikali ili kuhakikisha rasilimali zinazotolewa zinawanufaisha wananchi kwa ufanisi,” amesema Mahenge.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Justice Rutenge, amesema hii ni mara ya saba mfululizo kwa wiki hiyo kufanyika, na mwaka huu itakuwa chini ya kaulimbiu: “Njia gani tunaweza kutumia ili kufikia maendeleo.”

Ameeleza kuwa Azaki zimekuwa na mchango mkubwa katika kuandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, ambayo tayari imekabidhiwa serikalini na inasubiri uzinduzi rasmi. “Azaki zimekuwa mstari wa mbele kuibua mawazo, kushiriki kikamilifu na kuhakikisha dira hii inaakisi mahitaji halisi ya Watanzania,” amesema.

Maadhimisho hayo pia yataangazia masuala ya demokrasia, utoaji huduma bora, ushirikiano wa maendeleo, na ubia kati ya sekta binafsi na umma. Aidha, kutakuwa na mikutano ya kitaalamu, kliniki za kujengeana uwezo, na mijadala ya wazi.

Katika upande wa udhamini, Mkuu wa Kitengo cha Taasisi za Umma na Mashirika Binafsi wa Benki ya Stanbic Tanzania, Doreen Dominic, ametangaza kuwa benki hiyo imetoa shilingi milioni 40 kwa ajili ya kuunga mkono maadhimisho hayo.

“Huu ni mwaka wa nne mfululizo tunashirikiana na Azaki, tukiamini kuwa maendeleo ya kweli yanatokana na mazungumzo ya wazi, ushirikiano na kuaminiana,” amesema Dominic.

Naye Mkurugenzi wa Tanzania Bora Initiative, Ismail Biro, amesisitiza kuwa wiki hiyo itaangazia pia changamoto zinazozikumba Azaki na namna bora ya kuzitatua kwa kushirikiana, huku makundi maalum yakipewa kipaumbele katika mijadala.

Wiki ya Azaki inatajwa kuwa jukwaa muhimu kwa wote wenye nia ya dhati ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya taifa, huku FCS ikihimiza washiriki wote kujisajili mapema ili kupata nafasi ya kushiriki kikamilifu.



Prev Post Taasisi ya Thabo Mbeki, AngloGold Waja na Muamko wa Maendeleo Afrika
Next Post Waziri Mkuu Kumwakilisha Rais Samia Maonesho ya World Expo 2025 Osaka, Japan
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook