

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche amesema kuwa Kamati Kuu ya chama chake inatarajiwa kukutana jijini Dar es Salaam Jumatano Mei 21, 2025.
Heche aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wanachama wa kikundi cha Chadema Family wa Kijiji cha Kakola wilayani Kahama mkoani Shinyanga katika kikao cha ndani.
Amesema kikao hicho kitajadili mikakati ya chama ikiwemo muendelezo wa kampeni ya No reforms, no election ‘bila mabadiliko hakuna uchaguzi’ ambayo imefanyika kanda mbalimbali za chama hicho.
“Kuna watu eti wanadai Chadema inakufa…Chadema hii hii tunayoitisha mkutano wa hadhara saa 2:00 asubuhi na watu wanajitokeza hadi mtu unakosa pa kukanya ndio inakufa? Wanajidanganya sana,” amesema Heche.
Bila kutaja ajenda za kikao hicho, Heche amesema: “Mei 19, 2025 tunaenda Mahakama ya Kisutu kwenye kesi ya Mwenyekiti wetu Tundu Lissu na Mei 21 tutafanya kikao cha Kamati Kuu. Baada ya hapo tutaueleza umma nini kinafuata. Chadema siyo tu ni chama cha siasa, Chadema ni imani katika mioyo ya Watanzania wapenda haki na demokrasia.”
Amesema kikao hicho kitafuatiwa na kikao cha Baraza Kuu ambacho hata hivyo hakutaja kitafanyika lini.
“Wamemkamata na kumweka ndani Lissu (Tundu) kwa kesi ya uhaini wakidhani tutatetereka kwa kujifungia ndani kulia, sasa wanashangaa kuona kampeni ya No reforms, No election inachanja mbuga,” amesema Heche.
Akaongeza kwamba wana timu mbili ambazo ni ile anayoingoza yeye (Heche) na Katibu Mkuu, John Mnyika: “Zashambulia kila kona kudai mabadiliko.”
Amewahakikishia makada wa chama hicho kuwa hakuna nguvu ya dola, vitisho, kesi wala kuta za magereza zitakazowarejesha nyuma ari na nia ya Chadema kudai mabadiliko ya kisheria yatakayoweka sawa uwanja wa siasa kwa wagombea wa vyama vyote.
“Naapia mimi na viongozi wenzetu hatutarudi nyuma katika mapambano ya kudai haki na maisha bora kwa Watanzania,” ameapa Heche.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!