
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya uhamisho na uteuzi wa viongozi mbalimbali. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka, uhamisho na uteuzi huo ni kama ifuatavyo:
Rais amemhamisha kituo cha Kazi Mhe. Albert Gasper Msando kutoka Wilaya ya Handeni kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam.
Mhe. Japhari Mghamba Kubecha amehamishwa kutoka Wilaya ya Tanga kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Aidha, Rais amemhamisha Mhe. Dadi Horace Kolimba kutoka Wilaya ya Karatu kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga;
Rais Samia amemteua Ndg. Lameck Karanga Nganga kuwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu. Kabla ya uteuzi huu, Bw. Nganga alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Karatu.
Naye Ndg. Bahati Migiri Mfungo ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Karatu. Kabla ya uteuzi huu, Bw. Mfungo alikuwa Afisa Tarafa ya Mbuguni, Wilayani Arumeru.
Pia amemteua Ndg. Lazaro Jacob Twange kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO). Kabla ya uteuzi huu, Bw. Twange alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo.
Katika uteuzi mwingine, Rais amemteua Ndg. Andrew William Massawe kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA). Bw. Massawe anachukua nafasi ya Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohamed Chande Othman ambaye amemaliza muda wake.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!