

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewataka Watanzania kuishi kwa upendo na kushirikiana kwa maslahi mapana ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Amesema katika kilele cha maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano ambapo amewahimiza Watanzania kukumbuka kuwa kuwa Mwl. Julius Nyerere na Hayati Mzee Abeid Amani Karume waliunganisha Tanganyika na Zanzibar katika misingi ya umoja, amani, ushirikiano na kuheshimiana hivyo, muhimu kuendeleza misingi hiyo ili kuenzi Muungano.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Aprili 26, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Soko la Kilombero, Wilaya ya Arusha Mjini, Mkoa wa Arusha.
“Arusha mfanye kazi kwa kushirikiana, muijenge Arusha yenu mkumbuke kwenye nafasi zetu za uongozi mjue kesho hamtakuwepo mtaondoka, kila mahala ulipo acha alama njema itakayo kumbukwa na wengine. Sisi tuliopo leo tutakumbukwa kwa lipi, iwe changamoto tunapokumbuka miaka 61 ya Muungano tujue ni alama gani tutaacha kwa watoto wetu,” amesema Dk. Biteko.
Amesema katika kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2025 Watanzania waishi kwa kuvumiliana na kuheshimiana na kuwa wamoja kwa kuchagua viongozi wanaoweza kuwasilisha ajenda zao kwa wananchi.
“Hicho ndicho kiwe kipimo na viongozi tusitumie tofauti zetu kutafuta kura, usiende kanisani au msikitini kwako kutumia uhalali watofauti zetu kutafuta kura asitokee yeyote kufanya hivyo tuuenzi Muungano na Rais Samia ameapa kuulinda Muungano huu kwa wivu mkubwa,” amesema Dk. Biteko.
Dkt. Biteko amebainisha Watanzania wasiruhusu Taifa kugawanyika kwa sababu yoyote ile wakumbuke kuwa kama hakuna amani hakuna biashara wala maendeleo yanayoweza kufanyika.
Pamoja na hayo, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ndani ya kipindi cha miaka minne, imetekeleza miradi mingi na kusimamia sera na mikakati mbalimbali ili kuuletea maendeleo Mkoa wa Arusha huku akitaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni kuboresha miundombinu ya barabara, ambayo inaiunganisha Arusha na mikoa na maeneo yote ya kimkakati. Kwa mfano, Barabara Arusha- Namanga –ambayo inakwenda hadi Nairobi nchini Kenya.

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!