WAMEBEBA tena! Bayern Munich walitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga), mwishoni mwa wiki baada ya kuichapa VfB Stuttgart mabao 4-2, ukiwa ni wa 35 kwao tangu mfumo mpya wa mashindano hayo ulipopitishwa Agosti 28, 1962, ingawa rasmi ligi ilianza kuchezwa msimu wa 1963/64.
Na kwa kubeba ubingwa huo, Bayern Munich ambao mashabiki wao wamekuwa wakibeba mabango wakiita timu yako kwa kifupi (BAMU), ikiwa na maana ya vifupisho vya maneno ya mwanzo ya jina lake, imeendelea kuwa timu tishio zaidi katika mashindano hayo kati ya timu 18 zinazoshiriki kila msimu.
Kwa wingi wa makombe ya Bundesliga, Bayern inafuatiwa na Borussia Dortmund na Borussia Monchengladbach zilizobeba mara tano kila moja.
Straika Harry Kane alifunga bao lake la 32 msimu huu wa Bundesliga baada ya kuingia kipindi cha pili, huku Bayern wakionekana kuwa na uwezo wa kufunga mabao zaidi dhidi ya safu dhaifu ya Stuttgart. Ushindi huo uliwaweka Bayern pointi 15 mbele ya Borussia Dortmund walio nafasi ya pili, huku kukiwa na mechi nne zilizobaki, tofauti ambayo haiwezi kufikiwa. Bavarians walihitaji sare tu kuthibitisha ubingwa baada ya Dortmund kupoteza dhidi ya Hoffenheim siku moja kabla.
Hilo ni taji la 35 la ubingwa wa Ujerumani kwa Bayern ikiwa ni rekodi mpya likijumuisha lile la kwanza 1932. Mataji yote yaliyofuata yalikuja baada ya kuanzishwa kwa Bundesliga 1963.
Stuttgart walitangulia kufunga kupitia Chris Fuhrich dakika ya 21, lakini Bayern walijibu haraka kupitia Raphael Guerreiro, Nicolas Jackson na Alphonso Davies ndani ya dakika sita kipindi cha kwanza. Chema Andres alifunga bao la pili la kuvutia kwa Stuttgart dakika ya 88.
SHEREHE TULIVU
Wachezaji wa Bayern Munich walijipanga mbele ya mashabiki wao kusherehekea ubingwa huo, lakini hakukuwa na sherehe za kawaida za kumwagiana bia kama ilizoweleka na hiyo ni kwa sababu klabu hiyo bado ina malengo makubwa kwani wanaweza kushinda mataji matatu msimu huu.
Timu hiyo itakutana na Bayer Leverkusen kwenye nusu fainali ya Kombe la Ujerumani (FA), na pia ina mechi ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya mabingwa watetezi, Paris Saint-Germain.
Kocha Vincent Kompany alifanya mabadiliko mengi kwenye kikosi chake baada ya mechi dhidi ya Real Madrid wiki iliyopita, huku nyota kadhaa kama Manuel Neuer, Kane, na Dayot Upamecano wakianzia benchi. Serge Gnabry alikosa mchezo kutokana na jeraha la paja, ambapo Jamal Musiala aliandika historia kwa kuwa mchezaji wa pili mwenye umri mdogo kufikisha mechi 150 za Bundesliga kwa Bayern baada ya Uli Hoeness.
Bao la Kane lililokuwa la 51 msimu huu katika mashindano yote liliisaidia Bayern kuweka rekodi mpya ya mabao mengi zaidi katika msimu wa Bundesliga (109), ikivunja rekodi ya mabao 101 iliyowekwa na kikosi cha 1971-72 kilichokuwa na mastaa kama Franz Beckenbauer na Gerd Muller.
Baada ya mechi hiyo kiungo wa timu hiyo, Joshua Kimmich alisema: “Ni kitu cha kipekee sana, hasa msimu huu. Siyo rahisi kucheza kwa kiwango hiki (bora) baada ya mechi kubwa kama ile ya (Real) Madrid.” Kwa Bayern, huo ni mwanzo tu, lakini lengo lao kubwa sasa ni kumaliza msimu kwa mafanikio makubwa zaidi.
The post MAJABU YA HARY KANE …BAYEN WAKIBEBA UBINGWA WA 35 BUNDESLIGA…. appeared first on Soka La Bongo.











Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!