
NCHI 40 zimekutana kujadili namna ya kufungua tena njia muhimu ya usafiri wa baharini ya Strait of Hormuz, huku Marekani ikiwa haijashiriki katika mazungumzo hayo makubwa ya kimataifa.
Hatua hiyo inakuja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuonekana kujiondoa katika juhudi za kushughulikia mgogoro huo, akiziambia nchi washirika wake zijitafutie mafuta yao wenyewe na kwamba hakuna sababu kwa Marekani kuhusika katika kufungua njia hiyo.
Mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao uliongozwa na Uingereza na ulihusisha mataifa kadhaa makubwa barani Ulaya pamoja na nchi za Ghuba.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Yvette Cooper, alifungua kikao hicho kwa kulaani kile alichokiita uzembe wa Iran, akisisitiza kuwa kufungwa kwa njia hiyo kunaathiri hata nchi ambazo hazikuhusika moja kwa moja na mgogoro huo.
Tofauti na ilivyozoeleka, hakuna mwakilishi yeyote wa Marekani aliyeshiriki katika mkutano huo, hali inayoonyesha mabadiliko makubwa katika sera ya Washington kuhusu usalama wa kimataifa.
Katika hotuba yake ya televisheni, Trump alisisitiza msimamo wake huo, akiziambia nchi zinazotegemea mafuta yanayopita Hormuz kuwa zinapaswa kuyalinda na kuyathamini zenyewe.
Mbali na diplomasia, mkutano huo pia ulijadili uwezekano wa hatua za kijeshi ili kuhakikisha njia hiyo inafunguliwa na kubaki salama.
Cooper alisema kuwa mara tu hali ya mvutano itakapopungua, wataalamu wa kijeshi kutoka mataifa mbalimbali watakutana kupanga namna ya kuondoa mabomu ya baharini yanayodhaniwa kuwekwa na Iran, pamoja na kulinda meli za mafuta.
Strait of Hormuz ni mojawapo ya njia muhimu zaidi duniani kwa usafirishaji wa mafuta, hivyo kufungwa kwake kuna athari kubwa kwa uchumi wa dunia, hasa kwa nchi zinazotegemea nishati kutoka Mashariki ya Kati.
The post Mshtuko Kimataifa! Marekani Yakwepa Mkutano wa Hormuz, Nchi 40 Zakutana appeared first on Global Publishers.











Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!