
Shirika la anga za juu la Marekani, NASA, limeanza rasmi hatua mpya ya safari za binadamu kwenda mwezini baada ya kuzindua misheni ya Artemis II, ikiwa ni mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka 50 kwa binadamu kusafirishwa kuelekea mwezini.
Safari hiyo ya siku 10 imeanza Jumatano Aprili 2, 2026 jioni ikiwa na wanaanga wanne: Reid Wiseman, Christina Koch, Victor Glover pamoja na Jeremy Hansen kutoka Canada.
Akizungumza baada ya uzinduzi huo, msimamizi wa NASA Jared Isaacman alisema kuwa dunia inaingia tena kwenye enzi ya safari za binadamu kwenda mwezini.
“Baada ya mapumziko ya miaka 54, sasa tumerudi rasmi kwenye safari za kuwapeleka binadamu mwezini,” alisema.

Hii ni mara ya kwanza kwa roketi ya Space Launch System (SLS) pamoja na chombo cha anga cha Orion kubeba binadamu angani, hatua muhimu kuelekea lengo la kutua mwezini mwaka 2028.
Baada ya kufika angani, wanaanga hao wataanza kazi mara moja kwa kufanya majaribio mbalimbali ndani ya chombo hicho, ikiwemo:
- Mfumo wa maji ya kunywa
- Mfumo wa hewa (life support)
- Mfumo wa choo
Pia watafanya majaribio ya teknolojia muhimu kwa misheni zijazo ambapo watahitaji kuunganisha chombo chao na vyombo vitakavyowashusha mwezini.
Ndani ya saa 24 tangu uzinduzi, NASA inapanga kufanya operesheni muhimu iitwayo Trans-Lunar Injection (TLI), ambayo itapeleka chombo hicho moja kwa moja kuelekea mwezini.
Iwapo kila kitu kitaenda sawa, wanaanga watatumia takriban siku tatu kusafiri hadi mwezini.
Siku ya Jumatatu, timu hiyo inatarajiwa kuzunguka mwezi na kufika umbali wa maili 4,000 hadi 6,000 kutoka uso wa mwezi.
Katika hatua hiyo:
- Wanaweza kuvunja rekodi ya umbali mkubwa zaidi kuwahi kufikiwa na binadamu kutoka Dunia
- Watakuwa wa kwanza kuona upande wa nyuma wa mwezi kwa macho yao
Baada ya kukamilisha mzunguko huo, wanaanga watarudi duniani na kutua kwenye Bahari ya Pasifiki karibu na San Diego tarehe 10 Aprili.
The post NASA Yaandika Historia Tena, Yazindua Misheni ya Artemis II Kuelekea Mwezini appeared first on Global Publishers.










Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!