

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa taarifa rasmi kwa umma kikieleza kuwa amri ya zuio la Mahakama Kuu iliyokuwa ikikizuia chama hicho kufanya shughuli za kisiasa imekoma kisheria tangu tarehe 10 Desemba, 2025.
Taarifa hiyo imetolewa leo Januari 23, 2026, na Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Rugemeleza Nshala, ambaye amesema amri hiyo ilitolewa na Jaji Hamidu Mwanga mnamo Juni 10, 2025, na kwa mujibu wa sheria ilikuwa na ukomo wa miezi sita.
Dkt. Nshala ameeleza kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Madai (Civil Procedure Code), hususan Kanuni ya 3 ya Amri ya 37, amri ya zuio la muda haiwezi kudumu zaidi ya miezi sita isipokuwa kama kuna maombi ya kuiongeza, jambo ambalo halikuwahi kufanyika katika kesi hiyo.
“Ikiwa ni pamoja na masharti mengine ya kutunza hesabu na kutoa amana, Mahakama inaweza kutoa amri ya zuio kwa mujibu wa kanuni ya 1 au kanuni ya 2, na amri hiyo itakuwa na maisha kwa kipindi kilichotajwa na Mahakama, lakini kisichozidi miezi sita,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Ameongeza kuwa tafsiri ya kifungu hicho ilitolewa wazi na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania katika kesi ya African Trophy Hunting Ltd dhidi ya Mwanasheria Mkuu na Wengine (Civil Appeal No. 25 of 1997), ambapo Mahakama ilibainisha kuwa amri ya zuio inaweza kuongezwa, lakini kwa jumla isizidi mwaka mmoja.
Kwa msingi huo, CHADEMA imesisitiza kuwa hakuna zuio lolote la kisheria linaloendelea kuizuia kufanya shughuli zake za kisiasa nchini.
The post Nshala: Zuio la Mahakama Dhidi ya CHADEMA Limekoma Kisheria Desemba 10 appeared first on Global Publishers.






Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!