Search
Sign In
2 Register
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

FCC YASIFIWA KWA KUONGEZA UBORA

  • 79
Scroll Down To Discover

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga akizungumza na waandishi akiwa katika ziara ya kikazi ya kutembelea Tume ya Ushindani (FCC), Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Hadija Juma Ngasongwa, akizungumza na waandishi wakati Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga alipotembelea ofisi za FCC.

………..

NA FRANCISCO PETER, DAR ES SALAAM

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga amesema kuwa Tume ya Ushindani (FCC) ni taasisi muhimu sana kwa mustakabali wa taifa kutokana na jukumu lake la kudhibiti bidhaa bandia na kulinda maslahi ya mlaji.

Ametoa pongezi hizo leo Novemba 24, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati alipotembelea tume hiyo kwa lengo la kuzungumza na watendaji wake ili kuimarisha misingi ya utekelezaji wa majukumu ya FCC pamoja na Wizara kwa ujumla.

“Tume hii ya Ushindani ni muhimu kwa mustakabali wa taifa letu. Ina jukumu kubwa katika masuala ya udhibiti, kulinda walaji, kudhibiti bidhaa feki, kutoa elimu kwa umma pamoja na masuala mengine ya kibiashara ikiwemo muunganiko wa makampuni makubwa ili kuhakikisha yanaendelea kuwa shindani, yenye manufaa na yanayoweka ustahimilivu wa biashara,” amesema.

Mhe. Kapinga amesema : “Leo tumefika hapa na tumefanya kikao cha ndani kwa ajili ya kuimarishana katika utekelezaji wa shughuli zetu. Tume ya Ushindani (FCC) imekuwa ikifanya majukumu yake vizuri sana. Matokeo mengi yanayoonekana katika jamii ni kutokana na kazi kubwa inayofanywa na tume hii”.

Aidha, amesema kuwa ziara hiyo imelenga kuimarisha misingi iliyopo ili kuongeza ubora na ufanisi wa kazi, huku akibainisha kuwa Watanzania wanaitegemea Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia taasisi zake za udhibiti na uratibu, ikiwemo FCC ambayo mara kwa mara imekuwa ikiboresha utendaji wake ili kufikia matarajio ya walaji.

“Tumeendelea kujadiliana kuhusu masuala ya udhibiti na namna bora ya kudhibiti bidhaa feki. Kwa sasa tupo katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi na mazingira ya biashara yanatofautiana kila siku,” amesema Mhe. Kapinga.

Ameongeza kuwa mikakati mipya imewekwa ili kuongeza ufanisi na ubunifu, ikiwemo ushirikiano na sekta binafsi kwa ajili ya kuboresha utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo.

Mikakati ya kuongeza mapato ya nje

Waziri Mhe. Kapinga amesema moja ya mikakati ya wizara katika kuongeza mapato ya nje ni kuimarisha kongani za viwanda ili kuongeza uzalishaji, ajira na mapato ya ndani na nje.

“Pia tutaendelea kutekeleza sera zetu ambazo ni himilivu, pamoja na sera mpya kulingana na mabadiliko ya mazingira ya biashara,”

Amesema sekta ya viwanda na biashara ni sekta shirikishi inayohitaji uratibu mpana na inafanya kazi na sekta mbalimbali ili kupunguza urasimu na kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa wawekezaji, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Hadija Juma Ngasongwa, amesema hali ya biashara nchini inazidi kukua na FCC imehamia zaidi kwenye uratibu kuliko udhibiti pekee.

“Tunaendana na falsafa ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha taasisi hizi zinatoa majibu na kuondoa kero kwa wananchi, hasa katika masuala ya uwekezaji,” amesema.

Ameongeza kuwa uwekezaji umekua kwa kasi na FCC inaendelea kuchambua miamala ya muunganiko wa makampuni kwa lengo la kukuza mtaji na kuokoa ajira hasa katika viwanda vilivyokuwa vikionesha dalili za kushuka.

Aidha, amesema ziara ya Waziri na Naibu Waziri imewapa nguvu na hamasa ya kuendelea kufanya kazi kwa weledi na uadilifu ili kuwahudumia wafanyabiashara na wawekezaji kwa usawa.

“Ziara hii imetufariji sana. Katika taasisi 13 zilizo chini ya Wizara, leo ametutembelea na kujionea majukumu yetu. Kwanza tunaimarisha ufanyaji biashara uendane na nguvu ya soko kwa hatua ya ushindani bila kutumia hila au mabavu, bali kwa kufuata misingi ya usawa,” amesema Ngasongwa.



Prev Post PITIA VICHWA VYA HABARI KATIKA MAGAZETI YA LEO NOVEMBA 26, 2025
Next Post NGUVU YA PESAAA….WAARABU KUMNG’OA FEI TOTO AZAM KWA BIL 5 KASORO…ISHU IKO HIVI……
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook