
Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kuanza ziara ya kiserikali ya siku 3 katika Jamhuri ya Angola kesho April 07 hadi 09, 2025 kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, João Manuel Gonçalves Lourenço ambapo ziara hii inalenga kukuza na kuimarisha zaidi mahusiano ya kihistoria na kidugu kati ya Tanzania na Angola.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga leo April 06,2025, imesema akiwa nchini humo, Rais Dkt. Samia atapata fursa ya kufanya mazungumzo ya uwili na mwenyeji wake Rais Lourenço, kuhutubia Bunge la Angola, kuweka shada la maua katika Mnara wa Kumbukumbu wa Muasisi wa Taifa hilo Hayati Rais António Agostinho Neto pamoja na kutembelea kiwanda cha mafuta cha Luanda.
Uhusiano wa Tanzania na Angola uliasisiwa na Waasisi wa mataifa haya mawili Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Rais António Agostinho Neto waliokuwa na maono ya pamoja ya kuikomboa Afrika na Watu wake.
Uhusiano huu umeendelea kuimarika siku hadi siku na sasa unajikita katika kukuza uchumi hasa katika sekta za biashara, uwekezaji, maendeleo ya miundombinu, mafuta na gesi, madini, uchumi wa buluu, afya, elimu na utalii kama zilivyoainishwa kwenye Tume ya pamoja ya Ushirikiano, ziara hiyo itashuhudia pia uwekaji saini wa Hati za Makubaliano (MOU) katika masuala yanayolenga kufungua fursa za biashara na uwekezaji na jitihada za kuimarisha ulinzi na usalama.
Rais Dkt. Samia amealikwa pia na Spika wa Bunge la Angola, Carolina Cerqueira ambae nae pia ni Mwanamke, kuhutubia Bunge la nchi hiyo na atakuwa ni Rais wa kwanza Mwanamke kutoka barani Afrika kuhutubia Bunge hilo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!