

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajab Mabele, ametoa wito kwa Watanzania wote kuunga mkono bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi kwa kutumia malighafi za ndani, akisisitiza kuwa hiyo ndiyo njia sahihi ya kuongeza tija ya uzalishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Meja Jenerali Mabele alisema kuwa jukumu la kukuza bidhaa za ndani halipaswi kubaki mikononi mwa serikali pekee, bali ni la kila Mtanzania mmoja mmoja.
“Ni lazima tuamini katika uwezo wetu. Tunavyozalisha fanicha bora kwa kutumia rasilimali za hapa nyumbani, ni muhimu jamii nayo ione thamani ya kuvitumia,” alisema Meja Jenerali Mabele.
Katika maonesho hayo, JKT walitunukiwa tuzo ya uzalishaji bora wa fanicha na ubunifu wa ndani, kama sehemu ya kutambua mchango wao kwenye sekta ya viwanda vidogo na vya kati.
Kwa mujibu wa Mabele, JKT imekuwa mshiriki wa kudumu wa maonesho hayo kwa miaka mingi, na mwaka huu walionyesha bidhaa mbalimbali zikiwemo:
Fanicha za ndani na ofisini
Vifaa vya matumizi ya majumbani
Huduma za ulinzi
Zote zikiwa zimebuniwa na kutengenezwa na vijana wa JKT kwa kutumia rasilimali zilizopo nchini.
Amesisitiza kuwa kuunga mkono bidhaa hizi kunamaanisha kuunga mkono ajira kwa vijana, kukuza teknolojia ya ndani, na kuimarisha uchumi wa Taifa kupitia matumizi ya rasilimali asilia za Tanzania.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!