
Mgombea wa Urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) na Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu, amesema hatashiriki katika malumbano na watu wanaomkosoa au kumbeza kuhusu uamuzi wake wa kugombea Urais na kushindana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza jijini Dodoma mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mwalimu alijibu swali la wanahabari kuhusu kauli za kumbeza zilizotolewa na kada wa CCM na aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole.
“Ameyasema ayaseme tu, mimi siko hapa kujibishana na mtu yeyote. Haijawahi kuwa hulka yangu, sijawahi kujibishana na mtu wala kumbeza mtu. Acha waseme, ninaamini katika uhuru wa maoni. Sio leo tu, hata nitakapoingia madarakani watu watasema na kusema, lakini mimi nimejikita kwenye nini Watanzania wanataka,” amesema Mwalimu.
Mwalimu amesema kampeni zake zitalenga kutoa majibu na suluhisho la changamoto zinazowakabili Watanzania, badala ya kujihusisha na maneno ya kejeli au malumbano binafsi.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!