

Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, ameonyesha kutoridhishwa na tafsiri iliyotolewa na Wakili Shaaban Marijani kuhusu uamuzi wa Mahakama katika kesi ya mgawanyo wa rasilimali ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Wakili Marijani, ambaye anasimamia kesi hiyo, alieleza leo Julai 17, 2025 jijini Dar es Salaam kuwa zuio la Mahakama (kesi namba 8960/2025) linawahusu viongozi wote wa CHADEMA nchini – kuanzia ngazi ya taifa hadi matawi – kutoshiriki shughuli za kisiasa, ikiwa ni pamoja na kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu masuala ya chama.
Kati ya waliotajwa kwenye zuio hilo ni Bodi ya Wadhamini wa CHADEMA, Mwenyekiti wa Taifa, Makamu Mwenyekiti (Bara na Zanzibar), Katibu Mkuu na Manaibu wao, pamoja na viongozi wa ngazi zote waliopo kwa mujibu wa uteuzi au waliokaimu nafasi.
Hata hivyo, kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Wakili Mwabukusi ameonyesha kushangazwa na uamuzi huo, akisema:
“Hili litakuwa ni zuio la kipekee kabisa la upande mmoja kuwahi kutokea katika nchi za Common Law? Kazi ya zuio ni kulinda hali ilivyo (status quo), siyo kufuta au kuua uwepo wa taasisi. Mgawanyo wa matumizi ya Zanzibar una uhusiano gani na mkutano wa wanachama wa Busokelo? Tandahimba? Longido au Serengeti? Sasa huu ufafanuzi unajitanuaje? Jimbo linahusikaje na mgawanyo wa ruzuku?”
Akihoji zaidi, Mwabukusi alieleza kuwa ni jambo la kushangaza kwa kesi ya dharura kushindwa kusikilizwa kwa dharura, huku muda ukitumika kuandaa maelezo ya kina kuhusu zuio badala ya hatua za haraka kisheria.
Kauli yake imeibua mjadala mpana kuhusu tafsiri ya maamuzi ya mahakama na mipaka ya mamlaka ya Mahakama dhidi ya vyama vya siasa katika mfumo wa kidemokrasia.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!