
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi leo Juni 20, 2025 amefika nyumbani kwa familia ya marehemu Mobutu Malima eneo la Kishili, Nyamagana mkoani Mwanza, kutoa pole kufuatia msiba huo mzito.
Marehemu Mobutu Malima alikuwa Afisa Mwandamizi katika Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu (Bara), Makao Makuu ya CCM, Dodoma, na alifariki dunia tarehe 15 Juni 2025.
Katika salamu zake za pole, Dkt. Nchimbi alieleza masikitiko yake kwa niaba ya chama, akimtaja marehemu Malima kuwa alikuwa mtumishi mwaminifu, mwenye nidhamu, bidii na mchango mkubwa katika kuimarisha shughuli za chama nchini.
“Tunaungana na familia ya marehemu, ndugu, jamaa na wanachama wote wa CCM kuomboleza kifo cha ndugu yetu mpendwa Mobutu Malima. Ameacha pengo kubwa ambalo halitazibika kirahisi,” alisema Dkt. Nchimbi.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka kwa familia, mazishi ya marehemu Mobutu Malima yamepangwa kufanyika Jumapili, tarehe 22 Juni 2025 katika eneo la Ihayabuyaga, wilayani Magu, mkoani Mwanza.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!