

Mwanza, Juni 19, 2025 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Juni 19, 2025 amefungua rasmi Daraja la JP Magufuli lenye urefu wa kilomita 3.0, pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 1.66 katika eneo la Kigongo–Busisi, mkoani Mwanza.
Mradi huo mkubwa wa miundombinu unatajwa kuwa wa kihistoria katika kukuza uchumi wa Kanda ya Ziwa na kuimarisha usafirishaji kati ya mikoa ya Geita, Mwanza, Simiyu na maeneo jirani. Daraja hilo ni miongoni mwa madaraja marefu zaidi Afrika Mashariki, na linatarajiwa kubadilisha kabisa mfumo wa usafiri wa barabara na kupunguza utegemezi wa kivuko katika eneo hilo.

Akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kushuhudia uzinduzi huo, Rais Samia amesema:
“Daraja hili sio tu linawaunganisha wananchi wa Kigongo na Busisi, bali linaziunganisha fursa za kiuchumi, kijamii na maendeleo ya watu wa Kanda ya Ziwa. Ni ishara ya dhamira ya Serikali kuendelea kujenga Tanzania ya viwanda na uchumi jumuishi.”
Daraja la JP Magufuli limepewa jina hilo kwa heshima ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye alianzisha ujenzi wake kama sehemu ya ajenda ya kuimarisha miundombinu ya taifa.
Wananchi wa eneo hilo wameeleza furaha yao kwa hatua hiyo, wakisema sasa safari zao zitakuwa za haraka, salama na kwa gharama nafuu zaidi.


Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!