
ARUMERU: Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa salamu za rambi rambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, CCM Mkoa wa Mbeya na wananchi waliopoteza wapendwa wao katika ajali iliyotokea jana mkoani Mbeya na kusababisho vifo vya watu 28.
Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla alitoa salamu hizo za pole kwa niaba ya CCM amesema hayo leo Juni 8 alipokuwa akizungumza na wananchi katika eneo la USA River wilayani Arumeru mkoani Arusha akihitimisha ziara yake mkoani humo.
Akisalimia wananchi hao tayari kwa kuelekea mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kuendelea na ziara yake Makalla amesema jana majira ya Saa 1 jioni ilitokea ajali mbaya sana mkoani Mbeya na kupelekea kifo cha watu 28.
Makalla ameeleza kati ya waliopoteza maisha katika ajali hiyo 12 miongoni mwao walikuwa ni wanawake na watoto wawili na 16 waliobaki walikuwa ni wanaume na kuelekeza salamu za pole za chama hicho kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na makundi mengine tajwa.
Pia amesema mbali na hao waliofariki lakini bado kuna majeruhi ambao wanaendelea kutibiwa, pia alitoa pole kwao akisisitiza anawaombea wapate nafuu.
“Chama Cha Mapinduzi kinatoa pole sana kwa familia zilizopoteza ndugu zao na kwa familia ambao ndugu zao wanaendelea kutibiwa tunawaombea wapate nafuu, nikaona nitumie mkutano huu wa kwanza kabla sijaanza kusema nitoe pole na kauli yetu ni kazi na utu, utu ni pamoja na hili nililolifanya sasa la kutoa pole,” amesema Makalla.
Pia Makalla ameelekeza Jeshi la Polisi na usalama barabarani kuendelea kudhibiti ajali hizo zinazoendelea kutokea, pia madereva waelewe sheria za barabara na kuhakikisha ajali zinaepukika ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!