KOCHA mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amefanya tathmini ya mchezo wa Kariakoo Derby na kueleza kuwa licha ya sare ya suluhu dhidi ya Yanga SC, safu ya ushambuliaji ya timu yake imeonyesha maendeleo makubwa.
Barker amesema kikosi chake kilitengeneza nafasi nyingi, hasa kipindi cha kwanza, na kwamba ari na ubunifu wa wachezaji wake katika shambulio inampa matumaini makubwa kwa michezo ijayo.
“Tumetengeneza nafasi nyingi za wazi, na ingekuwa bora kama tungeweza kuzitumia vizuri. Namna wachezaji walivyoonyesha ubunifu na kupambana, inatupa motisha ya kuendelea kuboresha umaliziaji,” amesema kocha Barker.
Simba jana iliambulia alama moja pekee baada ya kutoka suluhu dhidi ya mtani wake wa jadi, Yanga, katika mchezo uliofanyika Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.
Barker amesema matokeo hayo hayakuwa sehemu ya mpango wake wa kupunguza pengo la alama katika msimamo wa ligi, huku akionyesha kutoridhishwa na sare hiyo ya bila kufungana.
“Malengo yetu yalikuwa ni kushinda ili kusogea karibu zaidi na Yanga, lakini mambo hayakwenda kama tulivyotarajia ndani ya dakika 90,” ameongeza.
Kocha huyo amekiri kikosi chake kilitengeneza nafasi kadhaa za wazi, hasa kipindi cha kwanza, lakini walishindwa kuzitumia ipasavyo na kujikuta wakikosa mabao ambayo yangewapa pointi tatu muhimu.
“Tumetengeneza nafasi za kutosha, hasa kipindi cha kwanza, lakini hatukuweza kuzimalizia kama tulivyopanga. Hilo linatupa maumivu kwa sababu tulikuwa na nafasi ya kufanya tofauti mapema,” ameongeza Barker.
Pamoja na kukerwa na matokeo, kocha huyo amesifia ari na kiwango cha wachezaji wake, namna walivyocheza dhidi ya timu yenye ushindani mkubwa kama Yanga ni jambo la kujivunia na linaonyesha maendeleo makubwa ya kikosi chake.
Barker ameongeza kuwa iwapo Simba wataendelea kuonyesha moyo huo wa kupambana na kuboresha umaliziaji wa nafasi, wana kila sababu ya kuamini kuwa matokeo mazuri yatakuja katika michezo ijayo.
The post SAFU YA USHAMBULIAJI YAMRUDISHA KOCHA DARASA appeared first on Soka La Bongo.






Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!