Search
Sign In
2 Register
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

HISTORIA, PRESHA DERBY YAAMUA HATMA YA WATANI

  • 21
Scroll Down To Discover

ILIKUWA miezi ikapita, masiku nayo ikapita, sasa imebaki saa 24 tu kabla ya kipyenga cha kuanza kupulizwa katika mchezo wa Kariakoo Derby kati ya Young Africans Sports Club na Simba Sports Club utakaopigwa Machi 1, 2026 katika Uwanja wa New Amaan Complex.

Mchezo huo unaotarajiwa kuanza saa 2:15 usiku, utawakutanisha Yanga wakiwa wenyeji wa pambano hilo, wakijipanga kuwakaribisha watani wao Simba katika dimba hilo la visiwani Zanzibar. Ni dabi inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini, huku kila upande ukiwa na sababu zake za kutaka ushindi.

Yanga wanaingia katika mchezo huo wakiwa na hali ya kujiamini zaidi, wakibeba rekodi bora ya hivi karibuni dhidi ya watani wao. Mabingwa hao wametoka kushinda mechi sita mfululizo za mwisho za Kariakoo Derby, jambo linalowaweka katika nafasi nzuri kisaikolojia.

Katika michezo hiyo sita, Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 5-1, 2-1, 1-0, 1-0, 2-0 na 1-0 dhidi ya Simba, wakionesha ubora na uthabiti mkubwa katika safu zote. Takwimu hizo zinaongeza presha kwa Simba, ambao wataingia dimbani wakihitaji kuvunja mwendelezo huo mbaya na kurejesha heshima yao mbele ya mashabiki wao.

Kamati ya Waamuzi ya Tanzania Football Federation (TFF) imemteua Nassoro Mwinchui kuwa mwamuzi wa kati wa pambano hilo. Atasaidiwa na Kassim Mpanga na Hamdan Said, huku Ramadhani Kayoko akiwa mwamuzi wa akiba. Uteuzi huo tayari umeanza kuzua mijadala miongoni mwa mashabiki wa pande zote.

Historia ya dabi hiyo iliyoanza mwaka 1965 imejaa kumbukumbu nzito zisizofutika. Miongoni mwa rekodi zinazokumbukwa hadi leo ni ile ya mshambuliaji wa Simba, Abdallah Kibadeni, aliyefunga mabao matatu (hat-trick) mwaka 1977, akiwa mchezaji pekee aliyewahi kufanya hivyo katika historia ya pambano hilo.

Katika mchezo huo wa mwaka 1977, Simba waliibuka na ushindi mnono wa mabao 6-0. Mbali na mabao matatu ya Kibadeni, mengine mawili yalifungwa na Jumanne Hassan, huku bao moja likiwa la kujifunga la beki wa Yanga, Seleman Sanga.

Dabi hiyo pia imewahi kushuhudia miujiza ya aina yake. Mwaka 2013 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Stadium, Yanga waliwahi kuongoza kwa mabao 3-0 kabla ya Simba kusawazisha na kufanya matokeo kuwa 3-3 katika mchezo uliobeba hisia kali kwa mashabiki.

Kadhalika, mwaka 1996 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Stadium, timu hizo zilitoka sare ya mabao 4-4, ukiwa ni miongoni mwa michezo yenye mabao mengi zaidi katika historia ya Kariakoo Derby.

Dakika 90 za Maamuzi
Licha ya takwimu, historia na rekodi zote, Kariakoo Derby hubaki kuwa mchezo wa dakika 90 zenye maamuzi yasiyotabirika. Mara nyingi matokeo hutegemea nidhamu, umakini na uwezo wa wachezaji kutumia nafasi wanazozipata.

Yanga wataingia wakisaka kuendeleza ubabe wao wa hivi karibuni, huku Simba wakisaka ushindi wa kurejesha matumaini na kuvunja mwiko wa kupoteza mechi sita mfululizo. Presha ni kubwa kwa wekundu hao ambao kwa muda sasa hawajaonja ushindi dhidi ya watani wao wa jadi.

The post HISTORIA, PRESHA DERBY YAAMUA HATMA YA WATANI appeared first on Soka La Bongo.



Prev Post SIMBA KAA TAYARI, PEDRO AFICHA KADI YAKE KUTUFU
Next Post KINACHOMSIBU MZIZE HUKO YANGA 😰😰….MASHABIKI MUOMBEENI TU….LA SIVYO MHHHH….
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook