OFISA Habari wa Yanga SC, Ali Kamwe, amewatumia onyo kali watani wao Simba SC, akieleza kuwa mshambuliaji wao mpya hatari, Laurindo Dilson Maria Aurélio maarufu kama Depu, anaonyesha alama za kuwaliza mapema wapinzani wao.
Depu aliyetua Jangwani katika dirisha dogo la usajili, tayari ameanza kuonyesha makali yake katika dimba.
Katika michezo minne aliyocheza hadi sasa, amefunga mabao sita na kutoa pasi moja ya bao, takwimu zinazozidi kuwapa matumaini mashabiki wa Yanga kuelekea michezo muhimu iliyo mbele yao.
Akizungumzia kiwango cha mshambuliaji huyo, Kamwe amesema hawana mashaka na uwezo wake, wakiamini Depu anaweza kubeba timu na kuamua matokeo hata katika mazingira yenye presha kubwa.
“Depu ni mshambuliaji tegemeo, anakupa matokeo katika presha. Tulikuwa kwenye wakati mgumu dhidi ya Namungo, lakini alikuja kutuliza jahazi na tukafanikiwa kuondoka na ushindi, bao la Depu lililosaidia Yanga kuondoka na alama tatu muhimu,” amesema.
Kamwe ameonyesha imani kubwa kwa nyota huyo, akitabiri kuwa katika mchezo ujao dhidi ya JKT Tanzania, Depu atafunga angalau mabao mawili, huku akiongeza kuwa si muda mrefu ataandika hat trick yake ya kwanza akiwa na jezi ya Yanga.
Mashabiki wa Yanga wanatarajiwa kushuka dimbani kesho katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam, huku macho na masikio yote yakiangalia Depu kuthibitisha maneno ya Ofisa Habari wao.
Baada ya mchezo huo, Yanga watakuwa na kibarua kizito zaidi katika Kariakoo Derby dhidi ya Simba SC, pambano litakalopewa Machi Mosi katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, mchezo unaosbiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini.
The post YANGA WAMTEGEMEA DEPU KUBEBA TIMU, DERBY appeared first on Soka La Bongo.






Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!