MSHAMBULIAJI wa Simba SC, Kibu Denis, anatarajiwa kushuka dimbani kwa mara ya mwisho kesho katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC FC, unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam.
Mchezo huo utakuwa fursa ya kipekee kwa Kibu kuwaaga rasmi mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi akiwa amevaa jezi nyekundu na nyeupe, kabla ya kufunga ukurasa wa safari yake ndani ya klabu hiyo aliyoidumia kwa nyakati tofauti zenye mafanikio na changamoto.
Baada ya kukamilika kwa mechi hiyo, Kibu anatarajiwa kuelekea nchini Libya kuanza maisha mapya ya soka akiwa chini ya klabu ya Al Nasr Benghazi, ambako anakwenda kukutana na mazingira mapya pamoja na changamoto nyingine katika taaluma yake ya uchezaji.
Taarifa zinaeleza kuwa uongozi wa Simba umekamilisha rasmi dili la kumuuza winga huyo kwenda Al Nasr Benghazi, hatua inayoweka kikomo cha ushirikiano kati ya klabu hiyo na mchezaji huyo ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.
Uhamisho huo umeifanya Simba kunufaika kifedha baada ya kuingiza kiasi cha dola za Kimarekani 300,000, sawa na Sh772,829,100 za Kitanzania, fedha ambazo zinatajwa kuwa sehemu ya mipango ya kuimarisha kikosi na uendeshaji wa klabu.
Kwa ujumla, uamuzi huo unaashiria mwanzo wa ukurasa mpya kwa Kibu na Simba kwa pamoja, huku klabu hiyo ikibaki kumtakia kila la heri nyota huyo katika safari yake mpya ya kikazi nje ya nchi
The post UWANJA WA KMC KUWA WA KIHISTORIA KWA KIBU appeared first on Soka La Bongo.






Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!