Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania Plc imezindua duka jipya la kisasa katika eneo la Mbagala Zakhem ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja Duniani.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kampuni akiwemo Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara, Bi Brigita Shirima, ambaye aliongoza zoezi la uzinduzi kwa kukata utepe, pamoja na Mkuu wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, Bi Happiness Shuma, na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja, Bi Belinda Wera. Pia walikuwepo washirika wa Vodacom wakiwemo wawakilishi kutoka kampuni ya Mayzon Group Limited wakiongozwa na Mtendaji Mkuu wake, Vishar Matambo.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Bi Brigita Shirima alisema:
“Katika kusherehekea Wiki hii ya Wateja, Vodacom Tanzania imekuja hapa Mbagala kusherehekea nanyi, lakini pia tumewaletea duka la Vodacom ambalo litaongeza urahisi wa kupata huduma zetu kwa ukaribu zaidi. Hili ni duka la kisasa lenye mazingira rafiki na jumuishi, ambayo yanawazingatia wateja wote ikiwemo wenzetu wenye ulemavu. Tunataka kila mteja wa Vodacom ajisikie kuthaminiwa na awe na uzoefu bora wa huduma kila siku.”

Kwa upande wake, Bi Happiness Shuma, Mkuu wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, alibainisha kuwa uzinduzi wa duka hilo ni sehemu ya mikakati endelevu ya Vodacom kuboresha huduma kwa wateja wake na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora katika maeneo yote ya nchi.

Uzinduzi huo umefanyika sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja Duniani, yanayolenga kutambua na kusherehekea mchango wa wateja katika mafanikio ya kampuni.
The post Vodacom yazindua Duka Mbagala ili kusogeza huduma kwa wateja wao appeared first on SwahiliTimes.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!