
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetoa tamko rasmi likieleza kuwa linaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya Ulinzi na Usalama nchini katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 28 na 29 Oktoba 2025, kama ilivyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi ya Taifa (INEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Katika taarifa iliyotolewa Tarehe 15 Oktoba 2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Kanali Bernard Masala Mlunga, Jeshi limeeleza kuwa kwa ujumla linaridhishwa na hali ya usalama nchini, ambapo kampeni za uchaguzi zinaendelea kwa amani na kwa kuzingatia sheria, maadili ya kisiasa, kuheshimiana na kuvumiliana miongoni mwa wagombea na wafuasi wao.
JWTZ limevitaka vyama vyote vya siasa, wagombea pamoja na wafuasi wao kuendeleza mazingira ya utulivu, ili taifa liendelee kuwa na uchaguzi huru, wa haki na wa amani. Pia, Jeshi limepongeza juhudi za Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kwa kusimamia vizuri hali ya usalama katika kipindi hiki muhimu kwa taifa.
Aidha, Jeshi limewapongeza wananchi kwa kutumia haki yao ya msingi ya kisiasa kwa kushiriki katika mikutano ya kampeni, kusikiliza sera za vyama na kujitayarisha kufanya maamuzi sahihi ya kuwachagua viongozi wa kuwaongoza.
Hata hivyo, JWTZ limeeleza kusikitishwa na ongezeko la taarifa potofu zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya watu wanaojiita wanaharakati, kutoka ndani na nje ya nchi, wakilenga kulihusisha Jeshi na masuala ya kisiasa kwa nia ya kuchafua taswira yake na kupunguza imani ya wananchi kwa chombo hicho cha ulinzi.
Jeshi limewahimiza wananchi kupuuza taarifa hizo za upotoshaji na kuendelea kuwa watulivu. Limeeleza kuwa taarifa zote rasmi kuhusu Jeshi zitakuwa zikitolewa kupitia Kurugenzi ya Habari na Uhusiano Makao Makuu ya JWTZ.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!