

Shughuli ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Amolo Odinga, imeanza leo katika Uwanja wa Kasarani, jijini Nairobi, ambapo maelfu ya wananchi na viongozi mbalimbali wamejitokeza kutoa heshima zao za mwisho.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria mapema ni Rais wa Kenya, Dkt. William Ruto, ambaye ameongoza viongozi wa serikali, wanasiasa, na mabalozi katika kuuaga mwili wa kiongozi huyo mkongwe aliyekuwa nguzo muhimu katika siasa na harakati za demokrasia nchini humo.

Pia, aliyekuwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, pamoja na viongozi wa vyama vya kisiasa, wabunge, na viongozi wa kidini wameonekana wakiwasili Kasarani kwa ajili ya kushiriki shughuli hiyo ya kitaifa.
Uwanja wa Kasarani umefurika wananchi waliovaa mavazi yenye picha na rangi zinazohusishwa na chama cha ODM, wakipaza nyimbo za kumkumbuka Raila kwa mchango wake mkubwa katika harakati za haki na usawa.
Ratiba ya mazishi inatarajiwa kuendelea kwa siku kadhaa, huku mwili wa Raila ukitarajiwa kusafirishwa hadi kijijini kwake Bondo, Kaunti ya Siaya, kwa ajili ya maziko yatakayofanyika mwishoni mwa wiki hii.


Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!