

Nairobi, Kenya – Aliyekuwa Waziri Mkuu na kiongozi wa upinzani wa muda mrefu, Raila Odinga, amemkosoa vikali Rais William Ruto kufuatia agizo lake la kuwaruhusu maafisa wa polisi kutumia nguvu, ikiwemo kuwapiga risasi miguuni waandamanaji waliohusika kwenye maandamano ya hivi karibuni.
Kupitia taarifa rasmi aliyoitoa Ijumaa, Julai 11, 2025, Raila alieleza kuwa agizo la kuwafyatulia risasi raia hata wale wanaodaiwa kuvunja sheria ni kinyume cha sheria, haki za binadamu, na misingi ya utawala wa kisheria.
“Katika maandamano au mazingira yoyote yanayohitaji utekelezaji wa sheria, maagizo ya kuwapiga risasi, kuwalemaza, au hata kuwasumbua raia ni makosa,” alisema Raila.
Raila, ambaye ni mmoja wa viongozi walioungana na serikali pana ya Ruto kupitia muungano wa kitaifa, alisisitiza kuwa utawala wa sheria ndio njia pekee ya kushughulikia raia wanaokiuka sheria, na sio matumizi ya nguvu kupita kiasi au hukumu za papo kwa papo.
Kauli hiyo ya Raila inakuja baada ya Rais Ruto, mnamo Jumatano, Julai 9, kutoa matamshi makali akiwatuhumu watu aliodai wanafadhili maandamano ya vurugu kwa lengo la “kubadilisha serikali kwa njia zisizo za kikatiba.” Katika hotuba hiyo, Ruto alionyesha hasira, akisema serikali yake haitakubali taifa kuyumbishwa.
“Nimekuwa nikivumilia, lakini sasa inatosha. Serikali haitavumilia njama za kuvuruga nchi,” alisema Rais Ruto.
Hata hivyo, Raila alitoa wito kwa serikali kufuata taratibu za kisheria, kuhakikisha wahalifu wanakamatwa na kufikishwa mahakamani badala ya kupigwa risasi.
“Ni lazima tuhifadhi utu wa kila Mkenya na kulinda haki za binadamu. Polisi wanapaswa kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, si vinginevyo,” alisisitiza.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!