DAR ES SALAAM
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amemwakilisha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Mhe. Dkt. Tulia Ackson katika kilele cha mashindano ya Miss Universe Tanzania 2025 yaliyofanyika Agosti 23, 2025 kwenye Ukumbi wa The Super Dome jijini Dar es Salaam.
Kupitia hotuba yake, Dkt. Tulia amesema kuwa mashindano hayo hayana budi kuangaliwa kama jukwaa la kukuza vipaji na fursa za vijana hususan wasichana. Aidha, ameeleza kuwa mshindi wa taji hilo ni zaidi ya mrembo, bali balozi wa heshima, maadili na mshikamano wa Watanzania. Pia alibainisha kuwa mashindano hayo yanatoa nafasi ya kuitangaza Tanzania kimataifa, hususan katika sekta za utalii na ubunifu, hivyo yanapaswa kuungwa mkono na wadau mbalimbali.
Dkt. Gwajima akisoma hotuba hiyo, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuendeleza mashindano hayo ili kuwawezesha washiriki kubadilisha vipaji vyao kuwa fursa za kiuchumi. Pia aliwahimiza Watanzania kuunga mkono washindi na washiriki wote kwa kuwa wao ni sehemu ya kizazi kipya chenye kujiamini, kinachothamini utamaduni wa Kitanzania huku kikilenga ushindani wa kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Emmanuel Ishengoma amesema kuwa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) lipo tayari kutoa ushirikiano kwa wadau wote wenye nia ya kuendeleza sanaa ya urembo. Alisisitiza kuwa mashindano hayo siyo suala la urembo pekee, bali pia ni sehemu muhimu ya kujenga ajira, kukuza vipaji na kuongeza mchango wa sanaa katika uchumi wa taifa.
Naye Muandaaji wa mashindano hayo, Millen Magese amesema kuwa Miss Universe Tanzania 2025 imeweka historia kwa kuja na dhima mpya ya kuwapa nguvu wanawake kupitia kauli mbiu ya “Empower Beyond”. Amesema kuwa mashindano hayo hayalengi tu urembo, bali pia yanawajengea washiriki ujuzi wa uongozi, kujitegemea na kuonyesha wanawake katika taaluma mbalimbali ili kuwahamasisha kufuata ndoto zao. Aidha, amebainisha kuwa mshindi wa mwaka huu ataenda kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya dunia yatakayofanyika nchini Thailand.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!