

Dar es Salaam, Agosti 1, 2025 — Shule ya Sekondari ya Makongo imeendelea kudhihirisha kasi yake ya maendeleo baada ya kufanya rasmi uwekaji wa jiwe la msingi kwa jengo jipya la bohari. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule, aliyekuwa mgeni rasmi, na akipokelewa na Mkuu wa Shule, Kanali Yuda Kitinya.

Shule hiyo kongwe, inayojulikana kwa nidhamu, uzalendo, na matokeo bora kitaaluma, imechukua hatua madhubuti za kuimarisha miundombinu yake kwa ajili ya manufaa ya wanafunzi na jamii inayozunguka. Jengo la bohari linatarajiwa kuwa nyenzo muhimu katika kuhifadhi chakula na vifaa vya shule, hasa wakati wa msimu wa mavuno.
Mgeni rasmi, Mhe. Saad Mtambule, alieleza kufurahishwa na dhamira ya shule hiyo katika kujitegemea na kubuni suluhisho za kimkakati. Aliahidi kuchangia mifuko 200 ya saruji kusaidia ujenzi wa bohari hilo, na kusisitiza kuwa iwapo mradi huo utafika hatua ya kuezeka, ofisi yake iko tayari kuendelea kushirikiana na shule kuhakikisha mafanikio yanafikiwa.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!