
Kijana Said Mrisho, ambaye miaka tisa iliyopita alinusurika kifo baada ya kufanyiwa ukatili mkubwa wa kutobolewa macho na kuchomwa visu sehemu mbalimbali za mwili wake, ameibuka tena na kuililia serikali na vyombo vya haki kumtendea haki anayostahili.
Akizungumza kupitia kipindi cha #Mapito, Said amesema kuwa licha ya tukio hilo la kikatili lililomwacha akiwa na ulemavu wa kudumu, aliyemdhuru – anayefahamika kwa jina la Scorpion – tayari alimaliza kifungo chake gerezani, huku sehemu ya hukumu iliyomwelekeza kumlipa fidia ya shilingi milioni 30 ikiwa haijatekelezwa kabisa hadi leo.
“Nilitobolewa macho, nikachomwa na visu mwili mzima, leo hii siwezi kujitegemea kama awali. Lakini hadi leo sijapata hata mia moja ya fidia ambayo mahakama iliamuru,” amesema Said kwa uchungu.
Said alieleza kuwa wakati Scorpion anaendelea na maisha yake uraiani baada ya kifungo, yeye bado anaishi kwa mateso makubwa, akiwa hana uwezo wa kuona, huku maisha yake yakitegemea msaada wa watu wa karibu.
Ameomba serikali, taasisi za haki za binadamu na viongozi wa sheria kuchukua hatua zaidi kuhakikisha maamuzi ya mahakama yanatekelezwa kikamilifu, na fidia anayostahili inalipwa.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!