WAKATI Fadlu Davids, akiwaaga rasmi wanachama na mashabiki wa Simba, Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars, Benni McCarthy ambaye pia aliwahi kuwa kocha wa washambuliaji kwenye klabu ya Man United ya Uingereza, na wa Timu ya Taifa ya Madagascar, Romuald Rakotondrabe, wametajwa kwenye orodha ya kutaka kuchukua mikoba yake.
Habari kutoka vyanzo mbalimbali ndani ya Simba na nje ya nchi, zinasema makocha hao wawili waliofanya vema kwenye fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), wamo kwenye rada za Simba, wakiongeza idadi ya makocha wanaotajwa kumrithi Fadlu, aliyeondoka ghafla kwenye timu hiyo.
McCarthy, ambaye kikosi chake kilitolewa kwa mikwaju ya penalti 4-3 dhidi ya Madagascar, katika mchezo wa robo fainali ya CHAN, vyanzo kadhaa vinamtaja kuwa yumo kwenye orodha ya wanaotakiwa kuvaa viatu vya Msauzi mwenzake, Fadlu.
Vyanzo vingine nchini Madagascar vinasema kuwa kocha Romuald, anawindwa na mabosi wa Simba kwenda kusimamia jahazi la Wekundu wa Msimbazi hao.
Raia huyo wa Madagascar, amejizolea sifa kemkem Afrika kwa sasa, baada ya kukiongoza kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo ambacho hakikudhaniwa hata kama kitavuka hatua ya makundi, lakini kikafika fainali ya CHAN na kutolewa kwa mbinde na Morocco kwa mabao 3-2, hali iliyofanya kipokelewe kama mashujaa kiliporejea nchini kwao.
Makocha hao wanaongeza idadi ya waliotajwa hapo awali, ambao ni Miguel Gamondi na Nasredine Nabi ambao wote wameshawahi kukifundisha kikosi cha Yanga.
Makocha hao wote wamepita kwenye Klabu ya Yanga kwa mafanikio makubwa. Nabi, raia wa Tunisia, aliifundisha Yanga kuanzia 2021 hadi 2023, huku ambapo kwa sasa si kocha tena wa Kaizer Chiefs baada ya kuondoka kwa makubalianao ya pande mbili hivi majuzi. Gamondi, raia wa Argentina, alikuwa Kocha wa Yanga, 2023 hadi 2024 alipotimkia Al Nasr ya Libya na sasa ni Kocha Mkuu wa Singida Black Stars.
Wakati hayo yakiendelea, Fadlu jana, aliwaaga wanachama na mashabiki wa Simba, akithibitisha rasmi kuwa hatokuwa sehemu ya klabu hiyo.
Hakurejea nchini wakati kikosi hicho kilipokwenda nchini Botswana kucheza mechi ya kwanza, hatua ya awali, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United, uliochezwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Obed Itani Chilume, mjini Francistown, na Simba kushinda bao 1-0.
Taarifa za uhakika zinasema kuwa kocha huyo anatarajiwa kutangazwa kuwa Kocha Mkuu wa Raja Casablanca, timu ambayo aliihudumu kama kocha msaidizi miaka miwili iliyopita.
“Kwa moyo mzito nasema kwaheri kwa Simba SC. Tangu nilipowasili, nilihisi mapenzi ya klabu hii kubwa na upendo wa mashabiki wake wa kipekee. Pamoja tulipambana, tukasherehekea, na tukakua imara zaidi kupitia kila ushindi na kila changamoto.
“Shukrani zangu za dhati kwa rais Mohamed ‘Mo’ Dewji kwa uongozi wake wa kuhamasisha, maono yake, na msaada wake wa kila mara.
“Kwa wachezaji, endeleeni kupambana, kuamini, na kulibeba benchi kwa heshima. Kwa benchi la ufundi na uongozi, asanteni kwa imani yenu na kujitolea bila kuchoka nyuma ya pazia.
“Kwa mashabiki wa Simba, ninyi ndio mapigo ya moyo ya klabu hii. Sauti zenu, nyimbo zenu, na shauku yenu isiyoyumba vitabaki milele kwenye kumbukumbu zangu. Asanteni kwa kuwapokea familia yangu kama wenu.
“Simba daima itabaki sehemu yangu, na naiombea klabu hii mafanikio yasiyo na kikomo, ustawi, na mataji mengi zaidi mbele ya safari. Asanteni sana, daima Nguvu Moja.” Aliandika Fadlu kwenye taarifa yake aliyoitoa.
Hata hivyo, rasmi uongozi wa Klabu ya Simba ulitoa taarifa kwa umma jana kuwa umefikia makubaliano ya kusitisha mkataba na Kocha Mkuu, Fadlu Davids, baada ya kuhudumu na timu hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja.
“Makubaliano haya ni matakwa binafsi ya Kocha Fadlu kwa uongozi wa klabu.
“Klabu ya Simba inamshukuru Kocha Fadlu kwa kuiongoza Simba kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya NBC. Uongozi wa klabu unamtakia heri na baraka Kocha Fadlu katika maisha yake ya soka nje ya Simba,” ilieleza taarifa hiyo.
The post MRITHI WA FADLU SIMBA HUYU HAPA….KOCHA WA MAN UNITED ATAJWA…. appeared first on Soka La Bongo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!