

Katibu wa Ngome ya Wanawake ya ACT Wazalendo, Fatma Abdulhabib Ferej, ameteuliwa rasmi kuwa mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya jina lake kupitishwa kwa kauli moja na Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho uliofanyika mkoani Dar es Salaam.
Uteuzi wa Ferej ulitangazwa rasmi usiku wa manane wa siku ya Alhamisi na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, ambaye aliwasilisha jina hilo mbele ya mkutano kwa niaba ya Halmashauri Kuu ya chama.
Baada ya utangazaji huo, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo (Bara), Isihaka Mchinjita, aliwahoji wajumbe wa Mkutano Mkuu kuhusu uamuzi wa uteuzi huo, ambapo wote waliitikia kwa sauti ya pamoja, “Ndiyo!”, kuashiria kuidhinishwa rasmi kwa jina hilo.
Ferej ni mwanasiasa nguli kutoka visiwani Zanzibar, mwenye rekodi ya uongozi na ushujaa katika masuala ya kijamii na kisiasa. Mwaka 2013, alitunukiwa Tuzo ya Mwanamke Jasiri na Serikali ya Marekani kupitia ubalozi wake nchini Tanzania.
Kwa uteuzi huu, Ferej atakuwa mgombea mwenza wa Luhaga Mpina, ambaye naye alipitishwa kuwa mgombea Urais kupitia chama hicho kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!