
Tanzania imeeleza kuziunga mkono nchi zinazoendelea zisizo na mlango wa bahari kutimiza matarajio na kukabiliana na changamoto zinazozikabili na kutoa wito wa kuchukua hatua za pamoja na kuufanya Mpango wa Awaza kubadilisha ahadi na kuleta matokeo chanya.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, ametoa kauli hiyo alipozungumza tarehe 6 Agosti 2025 kwenye Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Nchi Zinazoendelea Zisizo na Bahari unaofanyika mjini Awaza, Turkmenistan.
Prof. Godius Kahyarara amesisitiza juu ya umuhimu wa kubadilisha Mpango wa Awaza kutoka kuwa tamko la Mkutano huo na kuufanya kuwa ramani ya kuelekea kwenya matokeo chanya ya maendeleo jumuishi.
“Tanzania si nchi isiyo na bahari, lakini nafasi yetu ya kimkakati kama nchi yenye Bahari na njia ya usafiri inatufanya kuwa kitovu cha muunganiko wa kikanda katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika. Bandari zetu, njia za usafirishaji, na miundombinu ya usafirishaji hutumika kama mishipa muhimu kwa uchumi wa nchi kadhaa zisizo na mlango wa bahari, ikiwemo Zambia, Malawi, Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,” alieleza Prof. Kahyarara.
Alihimiza kuwa Tanzania itaendelea kujitolea kutoa suluhisho bora, salama na linalostahimili mabadiliko ya tabianchi kwa ajili ya kurahisisha biashara na maendeleo kwa majirani zake wasio na mlango wa bahari.
“Tunaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya uwekezaji kupitia Ukanda wa Kati na TAZARA, kuboresha Bandari ya Dar es Salaam, kupanua miundombinu ya reli na barabara, pamoja na kurahisisha taratibu za forodha mipakani kwa mujibu wa Mkataba wa WTO wa Kurahisisha Biashara na soko la eneo huru la Afrika (AfCFTA). Tunaamini kuwa kubadilisha njia za usafirishaji kuwa kanda za kiuchumi ni hatua muhimu kwa mageuzi ya kiuchumi, ushirikiano wa kikanda, na ustawi wa pamoja,” alisisitiza.
Alieleza kuwa Tanzania imedhamiria kuendelea kushirikiana kwa njia za uwili, ushirikiano wa Kusini kwa Kusini, ushirikiano wa pembe tatu na majukwaa ya kikanda ili kusaidia nchi zisizo na mlango wa bahari kuvuka vizingiti vya kimfumo na kuwa nchi zenye uhusiano wa moja kwa moja na masoko.
Prof. Kahyarara alisema Tanzania inasisitiza haja ya kuchukua hatua za pamoja ili kuhakikisha Mpango wa Awaza unakuwa siyo tu tamko la nia, bali ni ramani ya kweli ya mageuzi.
“Mkutano huu uwe chombo cha mabadiliko ambacho kitaashiria mwanzo mpya—ambapo maendeleo ya nchi yoyote hayatekwi na jiografia yake, bali mshikamano na maendeleo ya pamoja ndiyo yanayoongoza safari yetu ya pamoja kuelekea 2030 na baada ya hapo,” alisisitiza.
Alisisitiza kuwa Mpango wa Awaza haupaswi kubaki kama hati isiyotenda kazi, bali uwe ramani hai ya mageuzi inayoungwa mkono kwa vitendo na washirika wa maendeleo, taasisi za kifedha, na nchi jirani za pwani kwa pamoja.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!