Na John Bukuku – Dar es Salaam
Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imeeleza kuwa ina jukumu la kulinda fedha za wateja wanaoweka akiba katika taasisi za fedha, kwa kutoa fidia iwapo benki au taasisi husika itafungwa au kufilisika.
Akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo Nanemane kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Isack Kihwili, alisema fidia hiyo hutolewa kwa kiwango kilichowekwa kisheria ambacho kwa sasa ni Shilingi milioni 7.5 kwa kila mteja.
“Tunatoa kinga ya kifedha kwa mteja pale ambapo benki au taasisi ya fedha inapofungwa au kufilisika. Iwapo mteja alikuwa anadai chini ya kiwango hicho atalipwa kiasi chote, lakini kwa wanaodai zaidi, hulipwa kiwango cha juu na kilichobaki hutegemea mchakato wa ufilisi,” alisema Kihwili.
Isack Kihwili alieleza kuwa kuanzia Julai 2025, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha mabadiliko ya Sheria ya Benki na Utaratibu wa Fedha, ambayo yameipa Bodi hiyo jukumu jipya la kupunguza hasara kwa wateja kabla ya hatua ya fidia kuchukuliwa.
“Sasa tutakuwa tunakaa na kutathmini hali ya benki inayokaribia kufilisika ili kuona uwezekano wa kuisaidia kupitia mkopo, kuweka amana au kudhamini mkopo. Hii inalenga kuiwezesha benki kupata uhai na kuepuka kuanguka moja kwa moja,” alieleza.
Kihwili alibainisha kuwa baada ya benki kufungwa, Bodi hiyo hufuatilia mali za taasisi husika kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na kisha kuuza mali hizo ili kupata fedha za kulipa wateja waliobaki.
“Hii husaidia kuendeleza imani ya wananchi katika sekta ya fedha, hivyo kuhamasisha utamaduni wa kuweka akiba kwenye taasisi rasmi, jambo ambalo linachochea mzunguko wa fedha na kuimarisha uwezo wa taasisi za kifedha kukopesha,” alisema.
Kihwili alifafanua kuwa mfuko wa fidia unatokana na michango ya wanachama wa Bodi hiyo, ambao ni benki zote zilizosajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania. Alisema kuwa wateja wa benki hawachangii chochote katika mfuko huo.
“Michango hutolewa na benki zenyewe. Mteja wa kawaida halipii hata senti moja. Huu ni mfumo unaolenga kulinda mteja wa kawaida dhidi ya athari za benki kufungwa,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Bodi ya Bima ya Amana, mabadiliko hayo ya kisheria ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha na kulinda maslahi ya wananchi wanaotumia huduma rasmi za kifedha nchini.
Kihwili alisema mikopo au udhamini utakaopewa benki itakayokuwa hatarini utaambatana na masharti mahsusi ili kuhakikisha kuwa fedha zinazowekezwa zinatumika kwa ufanisi na kwa kulinda maslahi ya wadau wa sekta ya fedha.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!