

Rajab Ally Samatta, mtoto wa kwanza wa marehemu Mzee Ally Samatta, ambaye ni baba mzazi wa mchezaji wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Samatta , amefunguka kuhusu chanzo cha kifo cha baba yao kilichotokea mapema leo katika Hospitali ya Kilwa Road jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Global TV, Rajab ambaye pia ni msemaji wa familia, amesema kuwa marehemu baba yao alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari kwa muda mrefu, hali iliyosababisha changamoto za kiafya zilizompelekea kufariki dunia.
“Ni kweli baba yetu amefariki leo asubuhi. Amekuwa akisumbuliwa na kisukari kwa muda mrefu, na leo hali yake ilizidi kuwa mbaya akiwa hospitalini,” amesema Rajab kwa huzuni.
Taarifa zaidi kuhusu ratiba ya mazishi na shughuli nyingine za msiba zitatolewa na familia kadri mipango inavyoendelea.
Watu mbalimbali, wakiwemo mashabiki wa soka, viongozi wa michezo, wasanii, na wananchi kwa ujumla, wameendelea kuonesha mshikamano na kutoa pole kwa familia ya Samatta kupitia mitandao ya kijamii.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!