

Tehran, Iran – Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ameonekana hadharani kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mzozo mkubwa kati ya Iran na Israel, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.
Runinga ya taifa ya Iran ilimuonyesha Khamenei siku ya Jumamosi akiwasalimia waumini kwenye msikiti wakati wa maandalizi ya maadhimisho ya Ashura, siku muhimu kwa waumini wa madhehebu ya Kishia.
Mara ya mwisho Khamenei kuonekana hadharani ilikuwa kupitia hotuba iliyorekodiwa wakati wa kilele cha mzozo na Israel, ulioanza Juni 13, 2025 kipindi ambacho makamanda waandamizi wa jeshi la Iran na baadhi ya wanasayansi wa nyuklia waliuawa.
Israel inadaiwa kufanya mashambulizi ya kushtukiza yaliyolenga maeneo ya nyuklia na kijeshi nchini Iran. Iran ilijibu mashambulizi hayo kwa kulipiza kisasi kupitia mashambulizi ya anga dhidi ya Israel, hali iliyochochea mzozo mkali wa siku 12 kati ya mataifa hayo mawili hasimu.
Katika kipindi hicho cha vita, Khamenei alionekana tu kupitia ujumbe wa video kwenye televisheni, hali iliyozua uvumi kuwa huenda alikuwa amejificha katika kituo cha siri chini ya ardhi kwa sababu za kiusalama.
Hata hivyo, siku ya Jumamosi, vyombo vya habari vya serikali ya Iran viliripoti kwa uzito mkubwa ujio wake hadharani. Khamenei alionekana akiwa karibu na waumini, akimgeukia kasisi maarufu Mahmoud Karimi na kumtaka aimbie wimbo wa taifa wa Iran uitwao “O Iran”.
Wimbo huo, ambao unaakisi uzalendo na mshikamano wa taifa, ulichukua nafasi ya kipekee wakati wa mzozo wa hivi karibuni na Israel na sasa unaonekana kama alama ya umoja wa kitaifa.
Mwonekano huu wa hadharani wa Khamenei umeleta faraja kwa wafuasi wake, huku wengi wakichukulia hilo kama ishara ya uimara na uthabiti wa taifa hilo baada ya kipindi kigumu cha sintofahamu na mashambulizi ya kijeshi.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!