
Chama cha ACT Wazalendo kimethibitisha kuwa Mgombea wake wa Urais, Luhaga Joelson Mpina, amewekewa mapingamizi matatu ya uteuzi wake na Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na wagombea urais wa vyama vya NRA na AAFP.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa ACT Wazalendo, Shangwe Ayo, mapingamizi hayo yaliwasilishwa usiku wa Septemba 12, 2025 majira ya saa 2:36 katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa chama hicho.
Taarifa hiyo pia imesema mapingamizi hayo yanadai kuwa Mpina hana sifa za kugombea urais, hajadhaminiwa na chama cha siasa na kwamba hakuteuliwa kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama chake. Hata hivyo, amesema hoja hizo hazina msingi wa kisheria na ni “njama za makusudi” zinazoratibiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali yake.
“Tunafahamu kuwa mapingamizi haya ni hujuma zinazotokana na hofu kubwa waliyonayo CCM dhidi ya mgombea wetu ambaye anakubalika zaidi na wananchi kuliko mgombea wao,” amesema Shangwe.
Ameeleza kuwa chama kimechukua hatua za kisheria kwa kujibu mapingamizi hayo kupitia wanasheria wake, na majibu yatapelekwa ndani ya muda uliopangwa. Aidha, ACT Wazalendo tayari imefungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa Msajili wa Vyama uliomnyima utambulisho Mpina kama mgombea halali wa urais. Kesi hiyo imesajiliwa kwa hati ya dharura kwa namba 23438/2025.
Katika Taarifa hiyo, Act Wazalendo pia imetangaza kuwa chama hicho kitapinga uteuzi wa mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, kwa madai kuwa hakufuata katiba na kanuni za chama chake katika mchakato wa uteuzi.
Pingamizi dhidi ya Mpina limeibuka siku moja baada ya Mahakama Kuu kuamuru Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kupokea fomu zake za uteuzi na kuendelea na mchakato wa kisheria.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!