
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imekubali ombi la Serikali la kuwalinda mashahidi wake ambao ni raia wa kawaida katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Tundu Lissu.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Hussein Mtembwa, Agosti 4, 2025, baada ya kuwasilishwa hoja na Wakili wa Serikali Cuthibert Mbilingi, ambaye alieleza kuwa mashahidi hao ni raia wa kawaida wanaoweza kuhatarishiwa usalama wao endapo taarifa zao zitafichuliwa wazi wakati wa usikilizwaji wa kesi.
Kwa uamuzi huo mashahidi hao watalindwa kwa maana ya kutoa ushahidi wao kwa kificho (bila kuonekana), majina yao kutotajwa mahakamani wala taarifa zao zinazoweza kuwafanya wakatambulika, wao, familia zao, marafiki zao na watu wengine wa karibu yao.
Serikali iliwasilisha ombi hilo kwa mujibu wa kifungu cha 194 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), marekebisho ya mwaka 2025, kinachotoa mamlaka kwa mahakama kuruhusu ulinzi kwa mashahidi katika mashauri ya jinai yenye maslahi ya juu kwa usalama wa umma.
Ikumbukwe kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliahirisha kesi ya uhaini inayomkabili, Tundu Lissu, hadi tarehe 13 Agosti 2025 ili kuwapa nafasi upande wa Jamhuri kuhakikisha Mahakama Kuu inatoa uamuzi kuhusu maombi ya kulinda mashahidi.
Sasa serikali inatarajiwa kuwasilisha taarifa kamili kuhusu hatua ya uhamisho wa jalada la shauri hilo kutoka kwa Msajili wa Mahakama kwenda kwa Jaji Mkuu kwa ajili ya kupanga usikilizwaji wa kesi ya msingi.
Endapo taratibu zote zitakuwa zimekamilika ifikapo tarehe hiyo, Mahakama Kuu itaendelea rasmi na usikilizwaji wa kesi ya uhaini dhidi ya Lissu.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!