Search
Sign In
2Your Cart
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

CHUO CHA BENKI KUU CHATOA KOZI ZA MUDA MFUPI NA MREFU KWA WASHIRIKI WA EAC NA SADC

  • 39
Scroll Down To Discover

Na John Bukuku – Dar es Salaam

Katika kuhakikisha Taifa linakuwa na sekta ya fedha imara na madhubuti, Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT Academy) kimejikita kutoa mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu kwa ajili ya washiriki kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Julai 12, 2025, kwenye banda la BoT katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, CPA Mukrim Ramadhan, Mratibu wa Programu kutoka Chuo cha Benki Kuu, alisema chuo hicho kilianzishwa rasmi mwaka 1991 kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi wa Benki Kuu pamoja na wale waliokuwa ndani ya sekta ya fedha.

Hata hivyo, kutokana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii, chuo hicho kilisajiliwa rasmi kuwa taasisi ya elimu inayotoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi.

CPA Mukrim alisema kuwa kwa sasa, BoT Academy inatoa kozi mbili kuu za muda mrefu ambazo ni:

Stashahada ya Kawaida katika Uendeshaji wa Shughuli za Kibenki na Usimamizi (Ordinary Diploma in Banking Practice and Supervision), na

Stashahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Kibenki (Postgraduate Diploma in Banking Management).

Udadahili wa wanafunzi kwa kozi hizi uko wazi. Kwa kozi ya stashahada ya kawaida, waombaji wanatakiwa kuwa na ufaulu wa angalau principal pass moja na subsidiary moja. Kwa upande wa kozi ya postgraduate, waombaji wanatakiwa kuwa na shahada ya kwanza — iwe ya benki au fani nyingine yoyote.

 “Kozi zetu zinafundishwa na wataalamu waliobobea kwenye masuala ya fedha. Kwa mfano, tunapofundisha masuala ya masoko ya fedha, tunamleta mtaalamu anayefanya kazi hiyo katika taasisi ya kifedha – hii ndiyo maana ya competence-based training,” alisema CPA Mukrim. 

Katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT Academy) kilijipambanua kama taasisi ya kipekee inayotoa mafunzo ya fedha kwa ubora wa hali ya juu kwa Watanzania na nchi jirani.

Mbali na kozi za muda mrefu, Chuo hicho pia kinafanya vizuri katika utoaji wa kozi fupi. CPA Mukrim alieleza kuwa kozi hizo hutengenezwa kulingana na mahitaji halisi ya taasisi zinazohusika, baada ya kutembelea taasisi hizo na kubaini changamoto au uhitaji wa mafunzo.

“Tumeweza kutoa kozi za ithibati kwa watoa huduma ndogondogo za kifedha, baada ya kugundua changamoto nyingi zilizopo katika usimamizi na utoaji wa mikopo mitaani. Tumeona watu wengi kudhulumiwa na watoa huduma ambao hawajasajiliwa au hawafuati taratibu za Benki Kuu.” Amesema CPA Mukrim

Mukrim aliongeza kuwa pia wanatoa programu za ithibati kwa waelimishaji wa masuala ya fedha (Financial Educators Certification Programme) ambazo zinalenga kuwafundisha waelimishaji hao ili kukuza uelewa wa Watanzania katika masuala ya fedha.

BoT Academy hutoa pia kozi maalum za “tailor made”, ambazo hutolewa kwa taasisi zinazokuja zenyewe kuomba mafunzo maalum kutokana na changamoto walizonazo. Hizi ni kozi ambazo hazipo kwenye kalenda ya kawaida ya mwaka, bali huandaliwa kulingana na mahitaji ya taasisi husika.

Chuo hicho, kilichopo Capri Point, Mwanza, kwa sasa kimekuwa na mwitikio mkubwa wa washiriki si tu kutoka Tanzania bali pia kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na SADC kama Kenya, Uganda, Malawi, Zambia, Ghana na South Sudan.

Kwa mujibu wa CPA Mukrim, mwaka huu pekee chuo kimepanga kutoa zaidi ya kozi 57 za muda mfupi, ikiwa ni ongezeko kubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo idadi ya kozi hizo ilikuwa chache sana.

Hata hivyo, kwa wale wanaotaka kujiunga na chuo hicho, CPA Mukrim alisema wanaweza kutembelea tovuti rasmi ya chuo: academy@bot.go.tz kwa ajili ya kujisajili kwa kozi mbalimbali. Dirisha la udahili tayari liko wazi tangu mwezi Mei, na Watanzania wote wanakaribishwa kutumia fursa hiyo adhimu kujiendeleza kitaaluma.

Kwa ujumla, Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT Academy) kinaendelea kuwa nguzo muhimu katika elimu ya fedha nchini, kikitoa mchango mkubwa katika kukuza uelewa wa masuala ya kifedha miongoni mwa jamii na sekta mbalimbali. 



Prev Post Vodacom Tanzania na Benki ya Stanbic Wakabidhi Vifaa kwa Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalum Bariadi
Next Post SIKU YA KOCHA MPYA YANGA YATANGAZWA….CV YAKE BABU KUBWA HAKUNA TZ….
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook